Wednesday, February 1, 2012

KANUMBA, RAY BIFU PALE PALE...



Steven Kanumba.

Vincent Kigosi ‘Ray’.

KAULI ya utata iliyotolewa na staa wa filamu za Kibongo, Steven Kanumba juu ya bifu lake na swahiba wake Vincent Kigosi ‘Ray’ inadhihirisha wazi kwamba bado mambo hayajaisha na mtiti upo pale pale...

Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalum, Kanumba alipotakiwa kueleza juu ya bifu lake na Ray, alisema hana kinyongo naye, lakini haimaanishi kwamba wataishi kama marafiki.

UTATA
Mwandishi wetu alimwuliza msanii huyo juu ya bifu hilo baada ya kumuona Kanumba akimchukulia Ray tuzo iliyotolewa na Shirikisho la Filamu Zanzibar (ZIFF) katika hafla iliyofanyika ndani ya Ukumbi wa Club Maisha, Masaki, Dar wiki iliyopita.

“Mimi sina kinyongo na Ray, unajua sisi watumishi hatuna tabia ya kuwa na kinyongo, ndiyo maana ukaona hata tuzo yake nilimchukulia wakati amesafiri. Kuhusu kuwa karibu kama zamani muda ukifika tutafanya hivyo,” alisema Kanumba bila ya kufafanua zaidi.

Kwa kauli hiyo, inaonekana wazi Kanumba bado ana kitu moyoni na alipokea tuzo ya Ray kwa vile alitajwa na si kwa mapenzi yake.

KITENDAWILI CHA BIFU
Kwa muda mrefu wasanii hao wameripotiwa kuwa ndani ya bifu zito huku sababu zikiwekwa kapuni, lakini waliweka mambo sawa na kurekodi pamoja sinema ya Offside baada ya ile ya kwanza ya O’prah kufanya vizuri.

Hivi karibuni wamedaiwa kuingia tena kwenye bifu, huku sababu inayopewa uzito ikitajwa kuwa ni tambo za magari yao mapya ya kifahari ambapo kila mmoja anatangaza kwamba lake lina thamani zaidi.

Kitu cha kushangaza ni kwamba, kwa nyakati tofauti, wawili hao wakihojiwa kuhusu uwepo wa bifu hilo, hukanusha au kutotoa ushirikiano wa kutosha.

KALAMU YA MHARIRI
Kwenye chuki hakuna mafanikio, ikiwa ni kweli Kanumba na Ray mna bifu, ni vyema mkakutana na kuketi pamoja ili kuyamaliza.

Ninyi ni marafiki, mmetoka mbali lakini pia mpo chini ya mwavuli mmoja wa sanaa ya maigizo, upendo na mshikamano ndiyo nguzo kuu itakayowalinda.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...