Friday, April 27, 2012

MALI ZA KANUMBA: Mama, baba ngoma nzito...



MOSHI unafuka kuashiria kuwepo kwa moto kwenye mali zilizoachwa na Marehemu Steven Charles Kusekwa Kanumba kufuatia baba mzazi, Mzee Charles kuchezwa na machale ya kupigwa chini kwenye mirathi...

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mzazi huyo wa kiume amechezwa na machale hayo kufuatia tetesi kuwa mama wa marehemu, Flora Mtegoa yuko kwenye mchakato wa kufungua mirathi baada ya  arobaini ya marehemu lakini yeye hajaambiwa.

“Mimi nawaambia, mali za Kanumba ngoma nzito, maana mzee (Charles) kasikia kwenye magazeti kuwa mzazi mwenziye anataka kufungua mirathi mara baada ya arobaini ya marehemu lakini yeye hajui,” kilisema chanzo hicho.

BABA KANUMBA
Baada ya nyeti hizo, paparazi wetu alimsaka baba wa marehemu, Mzee Kanumba na kumuulizia kuhusu hali ilivyo katika mali za marehemu ambapo alisema:

“Mimi nazifahamu mali zote za marehemu. Ana magari, ana kampuni na viwanja viwili. Awali niliwasiliana na mama wa marehemu, akaniambia akiwa kwenye mchakato wa kufungua mirathi atajinijulisha lakini nasikiasikia ameanza mchakato kimyakimya, sitakubali.

“Hata hivyo, nafuatilia kwa karibu ili nione kama ni kweli, na kama ni kweli nitatoa ripoti kamili. Lakini pia baada ya arobaini nitaweka wazi jambo fulani ili jamii ijue.”

MAMA KANUMBA
Kwa upande wake, mama wa marehemu, Flora aliwahi kutaka kuwa mirathi itafunguliwa baada ya arobaini na kila kitu cha marehemu kitawekwa wazi.

“Kanumba anadai na kudaiwa, siku hiyo kila kitu kitakuwa wazi, hakuna kitakachofichika. Baba wa marehemu, kama atapata au hatapata itajulikana siku hiyo, ila marehemu kamuacha mdogo wake (Seth Bosco) ambaye atachunga mali zake maana kama ni kazi za filamu anazijua, alimfundisha,” alisema mama wa marehemu.

Aidha, kuna habari kuwa mama Kanumba aliwahi kuweka wazi kuwa marehemu hakuwa na mawasiliano mazuri na baba yake kwa miaka mingi hivyo hawezi kuwepo kwenye mirathi.

MALI ZA KANUMBA
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mazishi ya Kanumba, Gabriel Mtitu, marehemu hakuwa tajiri kwani ameacha magari matatu, viwanja kadhaa na shilingi milioni 40 benki. Kwa maana hiyo, nyumba aliyokuwa akiishi marehemu haiwezi kuwa kwenye mali kwa kuwa alipangisha.

OFISINI KWA KANUMBA
Kwenye ofisi ya marehemu, Sinza Mori (jirani na Meeda Bar) kuna vifaa vya kushutia filamu kama vile kamera, stendi, taa, maiki, kompyuta na gari la kubeba miundombinu inayohusu filamu aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T939 AVZ. Vyote kwa pamoja vina thamani kubwa ya fedha. Ofisi hiyo imeshaanza kazi.

UTATA WA GARI AINA YA LEXUS
Wakati huohuo, kuna utata wa gari la marehemu aina ya Lexus lenye usajili wa T750 AER ambalo awali Kanumba alidai alilinunua kwa shilingi milioni 78 lakini kufuatia kifo chake, zimeibuka taarifa kuwa gari hilo bado lina deni.

Inasemekana kuwa marehemu hakulinunua yadi gari hilo, bali alibadilishana na mtu kwa kutoa gari lake aina ya Toyota Harrier na kuongeza fedha kidogo, yeye akapewa Toyota Lexus.
“Lile Harrier, marehemu alimpa mtu akamwongeza na fedha kidogo, yeye akapewa Lexus, kwa hiyo bado anadaiwa kidogo,” kilisema chanzo.

Mama wa marehmu alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisisitiza mambo yote yatajulikana kwenye arobaini.

MIRATHI KWA MUJIBU WA SHERIA
Kwa mujibu wa sheria za nchi, mwenye haki ya kusimamia mirathi ya mtoto ni baba na mama bila kujali wanaishi pamoja au wametengana. 

UZOEFU
Miongoni mwa mambo yanayosumbua jamii ni migogoro inayohusu mirathi, hasa pale inaposimamiwa na ndugu wa kiume. Kwa hii ya marehemu Kanumba, kunaweza kuwa na tofauti kidogo kwani sehemu kubwa ya nguvu inaonekana ipo kwa mama wa marehemu kuliko baba.
Wakati tunakwenda mitamboni, kuna habari kuwa baadhi ya wanaharakati wamejipanga kuingilia kati mirathi ya marehemu Kanumba endapo italeta utata.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...