Wednesday, January 4, 2012

DIAMOND ATIWA MBARONI...




Asiyefunzwa na mamaye, ulimwengu lazima itamshikisha adabu, ‘bwa mdogo’, Naseeb Abdul ameota mapembe, umaarufu mbuzi alionao umempa kiburi, akajiona mbabe kuliko Tyson, akampiga mwandishi wa habari lakini mwisho akapewa kibano na kulala lupango.
Tukio hilo, ni nuksi ya kwanza kwa Diamond mwaka 2012, kwani baada ya kuibua rabsha nzito ya kumdhalilisha Mwandishi wa Habari wa Global Publishers & General Enterprises Ltd, Iringa, Francis Godwin, alishuhudia mkesha akiwa ‘ubayani’ a.k.a kwenye kinyesi.
Chanzo cha Diamond kuswekwa rumande na kuukaribisha mwaka akiwa lupango ni ujasiri wa kizamani alionao ‘janki’ huyo ambao ulimtuma kumpa kichapo Francis, kumnyang’anya kamera, kufuta picha na kuivunjilia mbali.



DIAMOND ALIITAFUTA SHARI IKIWA MBALI
Desemba 31, 2011, Diamond alitakiwa kutumbuiza kwenye shoo ya kuuaga mwaka kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.
Shoo hiyo, iliyoandaliwa na mwanamuziki wa siku nyingi wa Bongo Fleva, Mike Mwakatundu ‘Mike T’, ilishindwa kufanyika kutokana na muingiliano wa ratiba.
Kwa mujibu wa menejimenti ya uwanja huo, shoo ya akina Diamond ilitakiwa kufanyika kuanzia saa 8:00 mchana na kufikia tamati saa 12:00 jioni, kisha kupisha tukio lingine la mkesha wa mwaka mpya ambalo liliratibiwa na Umoja wa Makanisa.   
Tukio la mkesha, lilitakiwa kuanza saa 12:00 jioni hadi saa 6:00 usiku na mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Christine Ishengoma.

Hata hivyo, shoo ya mchana ilishindwa kufanyika baada ya Diamond kuchelewa kufika uwanjani.
Diamond, alifika uwanjani saa 11:50 jioni na mpaka anajiandaa kupanda jukwaani, tayari muda ulikuwa umemtupa mkono.
Baada ya mashabiki kutangaziwa kuwa Diamond hataweza kuimba kwa sababu muda umemtupa mkono, vurugu zilitawala, huku mwanamuziki huyo akilazimishwa apande jukwaani kwa nguvu.
Kutokana na hali hiyo, Diamond alipanda jukwaa lililokuwa limeandaliwa na Umoja wa Makanisa kwa ajili ya shughuli ya mkesha kwa lengo la kuwaridhisha mashabiki lakini menejimenti ya uwanja, ilimshusha haraka kwa sababu ilikuwa ni kinyume na makubaliano.
Wakati Diamond anashushwa jukwaani, paparazi huyo ‘alimfotoa’ za harakaharaka, kitendo ambacho mwanamuziki huyo hakukubaliana nacho.
Bila woga wala simile, Diamond alimvaa Francis na kumpa kipigo, kisha akamnyang’anya kamera, akafuta picha kabla ya kuipiga chini na kuivunja.
Katika tukio hilo, Diamond alisababisha upotevu wa kamera hiyo ambayo thamani yake ni shilingi 1, 500,000 simu aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 300,000, pia mwanamuziki huyo aliiharibu kompyuta mpakato (laptop) ya mwandishi huyo aina ya Acer.
Baada ya kadhia hiyo, paparazi huyo alikwenda kuripoti polisi kabla ya Diamond kubebwa msobemsobe hadi Kituo cha Polisi Kati alikolala kuanzia jioni ya Desemba 31, 2011 hadi Januari Mosi, 2012 mchana ambapo aliachiwa kwa dhamana.
Tukio hilo, kwa wengine limechukuliwa ni laana ya kusemwa vibaya na warembo ambao amekuwa akiwachanganya kimapenzi.
Hivi karibuni, ulizuka mzozo mkubwa baina ya ma-Miss Tanzania 2006-07, Wema Sepetu aliyebeba taji na mshindi wa pili, Jokate Mwegelo, ikidaiwa kwamba wote wawili, Diamond amewachanganya kimapenzi. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...