SAKATA la Morine Liyumba ambaye ni binti wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, kukamatwa na madawa ya kulevya ‘unga’, linawahusisha vigogo 10 Bongo.
Vyanzo visivyo na shaka vimetaja majina 10 ya vigogo ambao wanahusika katika mtandao ambao ndiyo uliokuwa unasafirisha madawa hayo ya kulevya kabla ya kukamatwa na Jeshi la Polisi Tanzania, Lindi.
Imedaiwa kuwa mtoto wa Liyumba na vijana wengine waliokamatwa ni ‘dagaa’ na kuongeza kwamba ‘papa’ wapo, siku wakitajwa taifa litatikisika kwa sababu majina yao ni makubwa na hadhi yao kijamii ipo juu.
“Hali ni mbaya, inasikitisha kwa sababu taifa linawaheshimu lakini wao ndiyo wahalifu. Wanaendesha mitandao hatari ya kuuza ‘unga’. Vijana ambao ni nguvu kazi wanaharibika na kugeuka mateja kwa sababu yao,” kilisema chanzo chetu ambacho kinahifadhiwa jina.
Chanzo kingine kiliongeza: “Inatakiwa safari hii serikali iwe makini kwelikweli. Imeshaamua, kwa hiyo isisite kuchukua uamuzi mgumu. Hatutaki kuona majina ya watu yanaachwa kwenye hili sakata la kukamatwa kwa mtoto wa Liyumba. Wote wafikishwe mahakamani.”
Majina ya vigogo 10 ambao wanadaiwa kuwemo kwenye mtandao uliokuwa unasafirisha madawa ya kulevya kabla ya kukamatwa Lindi wiki iliyopita lakini yanahifadhiwa kwa sababu ya kukwepa kuvuruga upelelezi wa kipolisi.
Morine, alikamatwa pamoja na mfanyabiashara wa magari, Ismail Adamu au kwa jina lingine, Athuman Mohamed Nyaubi, 28, raia wa Tanzania anayeishi Afrika Kusini.
Mwingine aliyekamatwa ni dereva, Hemed Said, 27, mkazi wa Mtoni, Temeke, Dar es Salaam na Pendo Mohamed Cheusi, 67, mkazi wa Lindi ambaye ni mmiliki wa nyumba ambayo ilikutwa na madawa hayo.
Kwa upande mwingine, wananchi waliozungumza na Amani, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete adumishe ulinzi kwa Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya Tanzania, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa.
Wamesema kuwa Nzowa anapambana na watu wazito ambao wana fedha nyingi lakini kazi yake ina manufaa makubwa kwa nchi kutokana na kitendo cha idara yake kuwaokoa vijana na janga la matumizi ya madawa hayo.
Nzowa aliwahi kuliambia BLOG hii kuwa amekuwa akipokea simu mbalimbali za vitisho kutoka kwa watu asiowafahamu kutokana na kazi yake.
Alipoulizwa anafanya nini ili kujihami na watu hao, alisema mara nyingi huwa anamtegemea Mungu. “Mimi namtegemea sana Mungu na ndiyo maana mara zote utanikuta nikiwa na Kitabu cha Biblia Takatifu na huwa nasoma Zaburi ya 23.”
No comments:
Post a Comment