Friday, November 18, 2011

Maajabu ya DUNIA: BINADAMU AGEUKA MTI




NI miujiza ya Mungu. Mitihani ipo kila kona kwa aina mbalimbali lakini hatutakiwi kukufuru. Tunapaswa kukubali matokeo na kuomba nusura kwa Muumba, kwani kazi yake haina makosa.

Binadamu ageuka mti! Unaweza kudhani ni simulizi ya miujiza lakini huo ndiyo ukweli. Ndugu yetu anayeitwa Dede Koswara, 41, raia wa Indonesia hivi sasa hatamaniki na wengi wanamwita ‘nusu mtu, nusu mti’.

Dede hajarogwa, isipokuwa amepata maradhi hayo baada ya kushambuliwa na virusi hatari wanaoitwa Human Papilloma (HPV), hivyo kubadili kabisa muonekano wake.


HALI HALISI YA DEDE
Alianza kushambuliwa na virusi hivyo akiwa na umri wa miaka 17, kwa maana hiyo ni tatizo ambalo ameishi nalo kwa miaka 24 sasa.

Ugonjwa ulianza kumshambulia kwenye mikono na miguu kabla ya kuhamia maeneo mengine ya mwili wake mpaka kichwani.
Tatizo ni kubwa kiasi kwamba vioteo vya upande wa mikono na miguu, vinashabihiana na miti mikavu, ubao mkavu ambao haujaondolewa magome yake.

Alishafanyiwa upasuaji mara tisa kuondoa tatizo hilo lakini mafanikio yakawa kupunguza kwa asilimia 95 kabla ya kuanza kuota tena.

Viotea ambavyo vinamfanya Dede aonekane kama mti, kitaalamu vinaitwa mapembe (cutaneous horns).
Hupatwa na maumivu makali kutokana na hali hiyo, hivyo kumfanya ashindwe kutembea au kufanya lolote lile.

Januari, 2008, akiwa na umri wa miaka 37, alifanyiwa upasuaji wa kwanza. Alipata nafuu na kueleza: “Namshukuru Mungu, angalau naweza hata kutembea.”

Alipopatwa na maradhi hayo, alikuwa anajishughulisha  na kazi za uvuvi lakini kwa sasa ameshindwa kumudu.

NGUMU KUPONA
Dk. Rachmad Dinata wa Hospitali ya Hasan Sadikin, Indonesia, amesema: “Hawezi kupona kwa asilimia 100 lakini maisha yake yanakuwa bora. Tumemtibu na kupunguza ukali wa ugonjwa, alikuwa anategemea watu kumfanyia kila kitu lakini sasa anaweza kula yeye mwenyewe, kuandika na kutumia simu ya mkononi.”

Dk. Anthony Gaspari, raia wa Marekani anayetokea Chuo Kikuu cha Maryland, amejitolea kufanya utafiti kubaini tiba kamili ya ugonjwa wa Dede. Taarifa yake ya awali, imeeleza kuwa virusi hao ambao ni adimu duniani, wamemfanya Muindonesia huyo aishiwe kabisa na kinga za mwili.

Dede ameweka tumaini lake kwa daktari huyo wa Marekani na ameeleza: “Naamini nitapona ila sijui lini. Kuna siku nitakutana na mwanamke na nitafunga naye ndoa. Natamani niwe baba wa familia na baadaye niwe na watoto. Napenda sana nibaki hai mpaka nitakapowaona wajukuu.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...