Wednesday, November 9, 2011

AFYA YAKO: UKOSEFU WA USINGIZI UNA ATHIRI AFYA YAKO



UNAWEZA kuwa makini sana na kila kitu unachochokula au unachokunywa kwa lengo la kulinda afya yako, lakini kama wakati wa kulala hupati usingizi, hali hiyo inaweza kuathiri afya yako.

Halikadhalika, kama mahali unapolala (kitandani au jamvini) na mazingira yake hayaendani na mahitaji ya mwili wako, huwezi kuwa na afya njema pia.

Mahali tunapolala pamoja na suala la kupata usingizi ni kitu muhimu sana kama kilivyo chakula. Utakumbuka kwamba karibu nusu ya maisha yetu tunayamalizia kitandani. Kama mtu ukijaaliwa kuishi duniani kwa muda wa miaka 60, kwa mfano, miaka 20 au 25 utakuwa umeitumia kwa kulala.

Unapolala, usingizi hufanyakazi ya kurejesha nguvu ya ubongo na mwili iliyopotea wakati wa mchana. Usingizi hurejesha upya nishati ya mwili na ubongo inayokuwezesha kupata akili ya kuainisha matatizo na kuyapatia ufumbuzi. Vile vile hukuwezesha kuamka asubuhi ukiwa na nguvu mpya ya kupambana na masuala mengine ya siku hiyo.

KWA NINI USIPATE USINGIZI?
Kama usingizi ndiyo muhimu kiasi hicho, kwa nini mtu usilale na kupata usingizi? Kuna sababu kadhaa zinazoweza kukufanya usipate usingizi, kuanzia chakula unachokula hadi mahali unapolala. Lakini habari njema ni kwamba kasoro zote unaweza kuzirekebisha na kupata usingizi mnono.

Kama una matatizo wakati wa kulala, kama vile kukosa usingizi, kuamka usiku mara kwa mara, kujisikia mchovu unapoamka asubuhi, au unahitaji kuboresha usingizi wako, kuna mambo mengi ya kufanya, yakiwemo haya yafuatayo:
HAKIKISHA unalala muda ule ule kila siku na muda mzuri ni saa 4:00 usiku.

JIEPUSHE kula vyakula muda mfupi kabla ya kupanda kitandani, hususan vitafunwa (snacks) vitokanavyo na nafaka na vyenye sukari. Badala yake kula vyakula vyepesi vya kuongeza protini mwilini, kama vile maziwa, n.k.

HAKIKISHA chumba unacholala kisiwe na baridi au joto sana. Wastani mzuri wa kiwango cha joto kinachokubalika kiafya ni nyuzi joto kati ya 18 na 21.

EPUKA kunywa kahawa au chai muda mfupi kabla ya kulala, vinywaji hivi huathiri usingizi kwa kiasi kikubwa.
HAKIKISHA unafanya mazoezi mara kwa mara, lakini siyo muda mfupi kabla ya kulala. Fanya mazoezi mapema na upate muda mrefu wa kupumzika kabla ya kupanda kitandani.

MWISHO kitanda, shuka na mto unaolalilia, hakikisha una ubora unaotakiwa. Shuka ya kujifunika na mto uliotengenezwa kutokana na pamba halisi (cotton wool) ni bora zaidi kuliko zilizotengenezwa kwa malighafi zingine, kama ‘polyester’, ‘synthetics’ n.k., ambazo zinadaiwa kuwa na kemikali zenye madhara kiafya.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...