KUNA mjadala mkali unaendelea kuhusu vinywaji baridi hususan soda, baada ya utafiti wa hivi karibuni kuonesha kuwa soda inaweza kuwa na madhara zaidi kiafya kuliko hata sigara!
Hii inaweza kuwa changamoto nyingine kubwa kumkabili binadamu katika masuala ya afya, kwani makampuni makubwa yanayotengeneza vinywaji baridi yanatumia mabilioni ya dola kila mwaka kujitangaza na kutoa misaada ya kijamii kutokana na mauzo yake bila kutaja madhara ya vinywaji vyao.
Soda inahusishwa na matatizo mengi ya kiafya kwa watoto na watu wazima, yakiwemo matatizo ya kuongezeka unene kupita kiasi (obesity), ugonjwa wa ini (liver disease) na hata tabia za vurugu (violent behavior). Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, unywaji wa vinywaji baridi mara kwa mara unachangia tabia ya ugomvi kwa asilimia kati 9-15!
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa nchini Marekani, soda huwekwa ‘fructose’ (sukari) nyingi ikiwa katika mfumo wa sirapu (fructose corn syrup) ambayo inaongoza kwa kusababisha magonjwa ya unene, kisukari, ugonjwa wa moyo na magonjwa mengine sugu yanayowakabili Wamarekani wengi hivi sasa na dunia kwa ujumla.
Dk. Mercola, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya lishe asilia na tiba mbadala anasema: ” Ninaposema kunywa soda ni hatari sawa na mtu anayevuta sigara au pengine zaidi, siyo jambo la kutia chumvi, bali ndiyo ukweli halisi”.
Dk. anaendelea kusema kuwa unywaji wa soda kwa njia nyingi ni mbaya kuliko uvutaji wa sigara, ila kutokana na kampeni kubwa ya matangazo inayofanywa na makampuni haya, inafanya vinywaji hivi vyenye sukari kuonekana havina madhara kwa watu wasio na hatia, hasa watoto wetu!
SABABU KUBWA YA KUIPIGA KIBUTI SODA
Unayesoma makala haya kuhusu madhara ya soda kwa mara ya kwanza bila shaka utakuwa unashangaa na kujiuliza; soda ina ubaya gani? Kwa mujibu wa Dk. Mercola, hakuna sababu yoyote ya kuendelea kunywa soda, labda ujikute uko katikati ya jangwa na hakuna kinywaji kingine isipokua soda!
Kiafya, unywaji wa soda au vinywaji vingine baridi vyenye ‘fructose’ una madhara. Unywaji wa kiasi cha kopo moja tu la soda kila siku, utakuongezea uzito wa mwili wa kilo 10 kila mwaka na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari (diabetes) kwa asilimia 85!
‘FRUCTOSE’
‘Fructose’ ni kirutubisho kilichomo ndani ya sukari na kiwango kinachowekwa wakati wa utengenezaji wa soda ni kingi kuliko kawaida. Inaelezwa kuwa miaka 100 iliyopita, Mmarekani mmoja alikuwa akitumia kiasi cha gramu 15 ya sukari (fructose) kwa siku, tena kwa kula matunda. Miaka 100 baadaye, (yaani hivi sasa), robo ya Wamarekani wote wanatumia kiasi cha gramu 135 (kutoka 15) kwa siku, tena kwa kunywa soda!
Ulaji wa sukari (fructose) kiasi cha gramu 15 kwa siku hauna madhara kiafya, labda uwe na ugonjwa wa kisukari (high uric acid levels). Hata hivyo, kwa kula sukari mara kumi zaidi ya kiwango cha gramu 15 kinachokubalika kiafya, inakuwa ndiyo chanzo cha unene wa kupindukia na magonjwa mengine hatari yanayoibuka mwilini (degenerative diseases).
Utafiti unaonesha kuwa vinywaji vingi baridi vina sukari nyingi kuliko wastani unaotakiwa. Badala ya kuwa na asilimia 55 ya ‘fructose’ na asilimia 45 ya ‘glucose’, vingi vina asilimia 65 ya ‘fructose’, ikiwa ni karibu asilimia 20 zaidi na inavyotakiwa.
Utafiti zaidi umeonesha kuwa ‘fructose’ ndiyo chanzo kikubwa cha tatizo la ugonjwa wa ini kwa watoto wengi nchini Marekani, ingawa hawatumii kilevi chochote (alcohol). Inaelezwa kuwa ‘fructose’ huleta madhara kwenye ini kama inavyofanya pombe.
Wiki iliyopita tulianza makala haya kwa kuangalia madhara yatokanayo na unywaji wa soda kwa wingi ambapo tuliona kuwa kiwango cha ‘fructose’ kinachowekwa kwenye vinywaji vingi baridi na hasa soda ni kikubwa. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa ‘fructose’ nyingi ina madhara mwilini na huwa chanzo cha magonjwa ya moyo, kisukari na ini. Wiki hii tunaendelea na sehemu ya mwisho kwa kuangalia athari nyingine, endelea…
NI KWELI SODA HUSABABISHA VURUGU?
Ni ukweli unaojulikana wazi kuwa lishe duni, hasa ile yenye kiasi kingi cha sukari ina athari kubwa kiakili. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na kuchapishwa kwenye Jarida la ‘Psychology Today’ nchini Marekani, umebaini kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya utumiaji wa sukari na hatari ya mtu kupatwa na mfadhaiko wa kiakili (depression) na ukichaa (schizophrenia).
Mlo wenye kiasi kingi cha sukari na ‘fructose’ kwenye vinywaji kama soda, husababisha uzalishaji mwingi wa ‘insulin’ ambako kunaweza kusababisha kushuka kwa kiasi cha sukari mwilini na kusababisha matatizo mengine yanayoweza kumfanya mtu kuwa na hasira, hamaki na mshituko.
Utafiti mmoja uliofanywa mwaka 1985 na kuchapishwa kwenye Jarida la ‘Abnormal Psychology’ nchini Marekani, ulibaini kuwa upunguzaji wa matumizi ya sukari una manufaa mengi katika hisia za mtu.
Katika utafiti huo, vijana waliokuwa na tabia mbaya na vurugu, walifanyiwa utafiti wa miezi mitatu kwa kupewa milo ya aina mbalimbali isiyokuwa na sukari na ilionekana kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kitabia kwa asilimia 44, ukilinganisha na wale waliokula milo au vinywaji vyenye sukari nyingi.
HIVYO NI KWELI SODA INA ATHARI KWENYE TABIA YA MTOTO?
Ni kweli soda zina athari kwenye tabia ya mtoto. Utafiti uliofanyika una sapoti maelezo haya kwa kubainisha kuwa unywaji wa mara kwa mara wa vinywaji baridi vyenye sukari, umehusishwa na vitendo vya vurugu kwa silimia 9 hadi 15 hata zikitumika jitahada zingine za kudhibiti hali hiyo.
WATAFITI WANAMALIZA KWA KUSEMA:
“Umebainika uhusiano mkubwa kati ya unywaji wa vinywaji baridi na vurugu, inawezekana ukawepo uhusiano wa moja kwa moja, labda kutokana na kiwango cha sukari na ‘kafeini’ kilichomo kwenye vinywaji hivyo au kunaweza kukawepo sababu nyingine ambazo hatukuzigundua kwenye utafiti wetu zinazo oanisha matumizi makubwa ya vinywaji baridi na tabia ya vurugu.
USHAURI
Watoto wetu hawezezi kujua vinywaji gani havina madhara kiafya kama mzazi hajawaambia na kuwaonesha kwa mfano kwa kutokunywa vinywaji hivyo. Kumfundisha mwanao vyakula na vinywaji vinavyokubalika kiafya ni jambo jema sana litakalomsaidia katika maisha yake yote na kamwe hawezi kupotoshwa na kampeni za matangazo.
No comments:
Post a Comment