Friday, June 1, 2012

MAHABA: Wanawake wanapenda kudanganywa



KAMA ilivyo ada tumekutana tena ili kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku. Nina imani kichwa cha makala kitakushtua, hasa wanawake. Siku zote kona hii imekuwa ikifanya uchunguzi wa kina na majibu yake huwa hayana shaka kwa jamii.
Kona hii imekuwa ikisisitiza umuhimu wa ukweli na uwazi katika mapenzi ambapo huwafanya wapenzi waondoe wasiwasi kwa wenza wao kutokana na kuwajua kiundani.
Kwa nini wanapenda kudanganywa?
Siku zote kiumbe wa kike hupenda vitu vizuri, kwa mfano kumpata bwana mzuri mwenye fedha na uwezo wa kitandani, hakuna mwanamke anayependa kinyume na hayo niliyoyataja, yakikosekana ataendelea kutafuta mtu sahihi atakayekubalika moyoni mwake.
Tupo pamoja? Najua unaweza ukajiuliza mbona wewe haupo hivyo na hata mpenzi wako hana kipato, pia hata maneno yake yamejaa maudhi lakini bado upo naye!
Siku zote utafiti wa jambo fulani unaweza ukafanywa na watu 10. Kama kuna wanawake 10, sita kati yao wakapenda kufanya kitu fulani wakati wengine wanne nao wakaegemea upande wa pili, wale sita ndiyo watatoa jibu la wanawake wengi wanapenda nini.
Katika uchunguzi wangu pamoja kuwasoma wanawake wengi ninapozungumza nao, nimegundua vitu hivi:
Vitu gani?
Kama nilivyosema awali mwanamke ni kiumbe kilichoumbwa kwa ajili ya kupamba dunia, hivyo kinapenda raha, shida ikitokea huwa bahati mbaya, sawa na kumfunga mbuzi mnyororo.
Tumeshuhudia wanaume wengi wa ukweli wakikimbiwa na wanawake baada tu ya kuonekana hawana vigezo, hasa uwezo wa kimaisha.
Pia tumeshuhudia wanawake wakiingizwa mkenge kutokana na kukutana na wanaume matapeli wa mapenzi kwa kujikweza wana fedha au nyadhifa kubwa serikalini. Hapo mwanamke huingia kichwakichwa na kuachwa solemba baada ya mhusika kukidhi haja zake za kimwili.
Tabia hii imewafundisha nini wanaume?
Tabia ya baadhi ya wanawake ambao ni asilimia kubwa, kupenda vitu vizuri, imesababisha kila mwanaume kutengeneza uongo ili ampate mwanamke fulani.
Wapo wanaoazima nguo, magari na hata vyumba, kwa kuhofia akienda alivyo, hawezi kukubaliwa. Kwa maana hiyo narudi tena kwenye kichwa cha habari kuwa wanawake wanapenda kudanganywa kuliko kuambiwa ukweli.
Madhara
yake nini?
Kutokana na watu wengi kuishi maisha ya maigizo ili wampate msichana, wasichana wengi huharibiwa ndoto zao za kuishi maisha mazuri na kuwa ‘vishata’.
Wengi wakishaujua ukweli kuwa mwanaume aliyenaye ni kula kulala, hana kazi, analala chumba cha watu watano, chumba alichotumia wakati wa kukutongoza ni cha rafiki yake, gari alilokuwa akitumia kukufuata pia la rafiki yake, husitisha mapenzi.
Inawezekana kabisa matangazo ya mwanaume mwongo yalisababisha hata kuachana na mpenzi wako mliyekuwa na malengo naye, wengine hufikia hatua ya kuvunja ndoa zao.
Nini cha kufanya?
Ni kweli kila kiumbe kinapenda maisha mazuri, lakini maisha hayo hayaji kwa lazima bali kwa kujituma, kuvumilia na kuikubali hali yoyote, si kutaka vizuri tu.
Penda ukweli na uwazi ili uingie kwenye penzi ukiwa unamjua kiundani mpenzi wako na kuamini ipo siku mtapata.
Usipende kuishi maisha ya mtu mwingine, acha tamaa, kama shoga yako kapata, subiri na wewe zamu yako, kwa vile Mungu si wa mmoja. Maskini naye ni mtu, msikilize ili kuepuka kulazimisha kudanganywa...

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...