Mtoto Kelvin Santos.
MTOTO wa miaka miwili aliyekuwa akiugua katika hospitali moja mjini Belem nchini Brazil akatangazwa na madaktari kuwa amekufa, ameibuka akiwa ndani ya jeneza na kukaa kisha kumuomba maji baba yake mazazi na muda mfupi baada ya kunywa maji, akafariki tena.
Tukio hilo lililoelezwa kuwa ni la miujiza lilitokea katika mji huo ulio kaskazini mwa Brazil na ni moja ya matukio yaliyotangazwa sana katika vyombo mbalimbali vya habari duniani ambapo mtoto Kelvin Santos aliyefariki hospitali kwa maradhi ya mapafu aliibuka na kukaa wakati waombolezaji wakitoa heshima za mwisho kwake.
Kwa mujibu wa taarifa, Kelvin aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Aberlardo kwa maradhi hayo ya mapafu, aliacha kupumua na daktari alipompima akaiambia familia kuwa amekwisha fariki dunia saa 1.40 jioni ya siku ya Ijumaa iliyopita na mwili wake ukakabidhiwa familia ukiwa umefungwa katika mfuko wa plastiki.
Habari zinasema familia ilichukua mwili wa mpendwa wao huyo na kuuweka katika jeneza tayari kwa mazishi kesho yake Jumamosi. Siku ilipofika jeneza lenye mwili wa Kelvin lilitolewa nje na kufunguliwa kwa ajili ya watu kutoa heshima zao za mwisho ndipo mtoto huyo alipoinuka na kukaa ndani ya jeneza na kumuita baba yake ambaye alipokwenda alimuomba maji ya kunywa.
Baba wa mtoto huyo, Antonio Santos alisema kila aliyekuwa kwenye msiba huo alipatwa na mshituko kutokana na muujiza huo. “Tulidhani ni muujiza kwamba mtoto wetu amefufuka, nilikimbilia jikoni kuchukua maji, lakini kabla ya kutekeleza ombi lake, alijilaza tena ndani ya jeneza kama alivyokuwa awali na jitihada za kumuamsha hazikuzaa matunda,” alisema mzazi huyo akiwa na uso wa huzuni.
Aliongeza kuwa baada ya hapo walimchukua Kelvin na kurudi naye hospitali na daktari alimpima tena na kuwahakikishia kuwa amekufa na hakuna namna. Alifafanua kuwa walirudi na maiti nyumbani ambako mazishi yalicheleweshwa kwa kuamini kuwa angeweza kufufuka tena lakini hadi saa 11 jioni alikuwa bado ‘kakauka.’
Santos alisema anashawishika kuamini kuwa kifo cha mwanaye kilitokana na uzembe wa madaktari kwani alipomfikisha hospitali wataalamu hao wa tiba walikaa naye kwa zaidi ya robo saa bila kumpa huduma yoyote, hivyo amefungua mashitaka polisi akitaka uchunguzi ufanyike kuhusiana na kifo hicho.
No comments:
Post a Comment