Wednesday, May 9, 2012

BABA ATOBOA SIRI YA KILICHOMPONZA KANUMBA




Marehemu Steven Charles Kanumba.

Mzee Charles Kusekwa.

Bi. Flora Mtegoa.

HUKU wingu zito likiwa bado limetanda juu ya kifo cha stadi wa filamu za Kibongo, Steven Charles Kanumba, baba mzazi wa marehemu, Mzee Charles Kusekwa ameibuka na kueleza mazito aliyoyataja kama ndiyo yaliyomponza mwanaye...
Akizungumza kwa njia ya simu wikiendi iliyopita kutokea Shinyanga, Mzee Kusekwa alisema wanaomtuhumu kuhusika na kifo cha mwanaye wanakosea kwa vile kuna jambo jingine nyuma ya pazia.

MWANZO WA JAMBO LENYEWE
“Ni vigumu kwa mtu ambaye una mtoto mkubwa unayemtegemea katika maisha halafu ushiriki kumfanyia mambo ya kishirikina, hilo haliwezekani hata siku moja.

“Watu wanatumia kigezo cha kuhitilafiana na mwanangu kuwa sababu ya kunihusisha na kifo chake. Yule ni mwanangu hata iweje, mtoto akikuchafua mkono kwa kinyesi huwezi kuukata mkono, hayo yalishapita sioni sababu ya kutaka kuhusishwa na kifo hicho.”

AANZA KUFUNGUKA
Akienda mbali zaidi, mzee huyo alisema tatizo lilisababishwa na tambiko ambalo yeye aliliita haramu kwa sababu halikuwahusisha wazee wa kimila wala kufuata taratibu zinazotakiwa. 

Alisema, tatizo ni kijana aitwaye Ayubu Mujungu ambaye ni mpwa wake (mtoto wa dada yake mzee huyo) aliyemchukua marehemu Kanumba na kumpeleka kwenye kaburi la babu yake kutambika kinyume na utaratibu wa mila zao.

“Kama ni matatizo ameyasababisha Ayubu ambaye kwa ujeuri tu alimchukua marehemu na kumpeleka Simiyu kwa ajili ya kutambika katika makaburi ya wazazi wangu.

“Binafsi miye na wazee wenzangu tulishangaa kuona kijana huyo akimchukua mtoto mwenziye (Kanumba) na kwenda naye kutambika katika makaburi bila ya kuwajulisha wazee.

“Kikwetu suala la matambiko hufanywa kwa taratibu maalum tena chini ya usimamizi wa wazee. Siyo mtu yeyote anaweza kwenda kufanya tambiko,” alisema.

ALIKIUKA MASHARTI
Alisema jambo jingine linalomfanya ahusishe tambiko la Kanumba na Ayubu katika kifo hicho ni kitendo cha marehemu kukiuka masharti ya kufanya tambiko kwa kuvaa mavazi siyo.
“Kuna kosa lingine Kanumba alilifanya, alivaa nguo nyeusi ambazo wazee wanasema kuwa haziruhusiwi kwenda nazo huko,” alisema.

Mzee Kusekwa alisema kuwa matokeo ya kukiuka mavazi, baada ya Ayubu na Kanumba kufika makaburini walikutana na vitu vya ajabu ambavyo mpaka leo ni Ayubu tu ndiye anayevijua lakini hataki kuviweka wazi.

Alizidi kuweka wazi kuwa ili kuwafunga midomo watu waliokuwa kwenye eneo la makaburi na kushuhudia maajabu yaliyowatokea wawili hao, waliwapa shilingi laki moja ili wasiseme.
“Hicho ndicho kilichosababisha kifo cha Kanumba kwa kuwa walikwenda kufukia vitu kwenye kaburi. Baada ya tukio lile mwanangu aliporejea Dar ndiyo akapata matatizo,” alisema.

KUHUSU MALI ZA KANUMBA
Mzee Kusekwa alisema muda wowote wiki hii atatua jijini Dar es Salaam kufuatilia suala la mali za mwanaye ambazo anadai amesikia zimeanza kuuzwa kiaina.

“Kuna kesi nimefungua Mahakama Kuu kuhusu kuzuia mali za mwanangu kuuzwa, hilo ndilo haswa linalonileta Dar. Kuna watu wanasema eti kwa mila za Kisukuma sistahili kuwa mrithi kwa sababu sikumtolea mahari mama Kanumba, hao wanakosea sana.

“Duniani kote watu wameshindwa kufananisha thamani ya fedha na uhai wa mtu, hakuna anayejua thamani ya mbegu ya Kanumba, hivyo kama sikumtolea mahari mama yake siyo sababu ya kunizuia kurithi mali za mwanangu. Mimi ndiye msimamizi wa mirathi,” alisema.

AMCHAMBUA AYUBU
Mzee Kusekwa alisema, chokochoko zote hizo amezileta Ayubu ambaye ni mtoto mdogo, akasema yeye (Ayubu) hajui mzee huyo na mama Kanumba walikutana wapi na walioana au hawakuoana.
Ameongeza kuwa Ayubu ni mtu wa kuchunga sana kwa kuwa tayari ameshajipendekeza kwa mama wa marehemu ili atajwe kama msimamizi wa mirathi wakati si mtu wa ukoo wao.

AMSHAURI MAMA KANUMBA
Katika kile kilichoonekana kutuliza hali ya hewa, mzee Kusekwa alitoa maneno aliyosema kuwa ni ushauri kwa mzazi mwenzake, Flora Mtegoa.

“Namsihi mzazi mwenzangu asisikilize maneno ya Ayubu maana ni mchonganishi, sisi tulishafanya kikao cha wanandugu lakini hakutokea, tukamtafuta na polisi kutokana na maneno yake akajificha uvunguni, bahati mbaya hatukuwa na hati ya kuingia ndani,” alisema na kuongeza:

“Aache kuamini ushirikina kwa kusema mtoto amechukuliwa msukule, hakuna msukule hapo ni matatizo ya tambiko. Kikubwa kwake kwa sasa ni kujenga imani kwa Mungu kwa kuwa ndiye aliyemchukua kiumbe wake.”

AYUBU KIKAANGONI
Tukiongea na Ayubu kwa njia ya simu na kuzungumza naye kuhusiana na madai hayo ya mjomba wake ambapo alitoa ushirikiano wa kutosha.

Kwanza, alianza kwa kukiri kuongozana na merehemu Kanumba kwenye makaburi yanayozungumziwa, akasema aliyewaagiza kufanya hivyo ni mama wa staa huyo Bi. Mtegoa.

“Tangu mwaka jana, mama Kanumba aliniagiza nimpeleke ndugu yangu katika makaburi na siyo kutambika bali ni kwenda kuyafagilia, hivyo Machi mwaka huu ndiyo tukatimiza,” alisema.
Kuhusu kutokewa na kitu kibaya makaburini hapo, alikanusha ingawa alikiri kumpatia fedha dada yake anayemfuata aitwaye Lucy ambaye ni mlemavu wa miguu.

“Hatukuwa tunamhonga, hapana. Yule ni dada yangu, tena anayenifuata mimi, tuliamua kumpa fedha kwa ajili ya kujikimu. Hata hivyo si laki moja kama alivyosema mjomba, ilikuwa ni shilingi 80,000.
“Tena nakumbuka mimi nilitoa 50,000 na Kanumba akatoa 30,000 fedha ambazo hazikuwa na sharti lolote lile.”

KUHUSU KANUMBA KUVAA NGUO NYEUSI
“Kanumba alivaa suruali ya jeans, rangi siikumbuki vizuri lakini haikuwa nyeusi na shati la rangi ya kaki. Hakuvaa nguo nyeusi kabisa.” 

Madai ya mzee Kusekwa kuwa anajipendekeza ili awe mrithi wa mali za marehemu Kanumba, Ayubu alisema si ya kweli na kwamba amejijenga vizuri kimaisha na si kutegemea mali za urithi.

“Nina pikipiki, gari, nyumba na ninaendesha biashara zangu mwenyewe, sina shida na mali za marehemu. Kwanza nafahamu kuwa mwenye haki ya kurithi ni mama mzazi wa Kanumba. 

“Hata huko kuondolewa katika ukoo ni watu wachache tu waliokutana kutokana na ushawishi wa baba Kanumba na sijapewa taarifa yoyote kwa kuwa aliyepangwa kuniambia, Elius Meshack hajaniambia chochote mpaka sasa.”

Ayubu alisema anashukuru kuwa yeye amemzika ndugu yake, amemuona kwa mara ya mwisho wakati alipomvalisha nguo na kumuwekea Biblia katika jeneza lake.

MAMA KANUMBA ANENA YAKE
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa marehemu amezungumza kuhusu suala la mzazi mwenzake kuharakisha suala la mali za Kanumba huku akisisitiza ni mapema sana.

Akizungumza kwa uchungu, nyumbani kwa marehemu Sinza jijini Dar es Salaam wikiendi iliyopita, mama huyo alisema mzazi mwenzake aache kuzungumzia kuhusu mali kwa wakati huu kwa vile ni mapema sana.

“Mimi nina uchungu na mwanangu, lakini mwenzangu naona anajali zaidi mali. Mimi ninalia, bado nipo kwenye msiba, yeye anasherehekea. Ndiyo maana hakuja msibani, mimi nimefika kumzika mwanangu, lakini siku chache baadaye, tayari anasema anazijua mali za marehemu.

“Sina haja na mali za Kanumba, nina nyumba, kazi na mali zangu nyingine, kwa nini nigombee mali? Nilitamani sana mwanangu anirithi mimi na siyo mimi nimrithi yeye.

“Ninatambua kuwa yeye ni baba wa marehemu, hilo halina ubishi, lakini atulie kwanza. Hata arobaini bado tunazungumzia mali, za nini? Halafu haya mambo yanakwenda kisheria, muda ukifika tutafungua mirathi mahakamani. Nipo tayari kusimama naye na siyo kulumbana kwenye” alisema Flora.

Akaongeza: “Hata ukiangalia sababu ya kutokuja kumzika mtoto haikuwa na maana. Mimi nilipopata taarifa mara moja nilifika, lakini mwenzangu akasubiri kamati ya mazishi impatie utaratibu na nauli. Utawezaje kusubiri kamati wakati umefiwa na mwanao?

“Kitu cha kushangaza alitumiwa nauli lakini hakufika kwa visingizio ambavyo mimi naviona havina maana. Hebu angalia, mfano alisema eti anaumwa, mbona alitumiwa nauli ya ndege? Usafiri wa ndege una shida gani? Ndiyo maana mimi nasema wakati mimi maumivu yangu yakiwa kwenye msiba, mwenzangu anawaza kupata mali, sasa asubiri muda ufike.”

Bi. Flora alikuwa katika sura ya majonzi muda wote, alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, lakini hali ilibadilika ghafla katikati ya mahojiano baada ya ndugu zake waliofika kumpa pole nyumbani hapo.

Ni kama msiba ulianza upya, maana alishindwa kujizuia na kuangua kilio, hivyo kusababisha wageni hao kujumuika pamoja kulia.

KALAMU YA MHARIRI
Kanumba amefariki dunia, ameshazikwa. Hakuna wa kubadili ukweli huu. Ni vyema sasa wazazi wakakutana na kujadiliana pamoja kuhusu suala la mirathi na kuacha kutupiana lawama. Majadiliano yenye usawa ni bora zaidi ya malumbano.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...