Tuesday, February 21, 2012

RIPOTI NZITO: UTAJIRI WA KUTISHA WA WACHUNGAJI...



http://en.hummer-cars-club.com/graphics/classifieds/45/full/hummer-08er-h2-6-2l-t1-bremrhvn-1.jpg
Usafiri wa Mchungaji.

Usafiri wa Muumini.

Nyumba ya Mchungaji.

Nyumba ya Muumini.

RIPOTI nzito inayohusu utajiri wa kutisha kwa baadhi ya viongozi wa dini  wakiwemo  wachungaji na maaskofu  na kuweka  utofauti mkubwa wa maisha baina ya waumini, umezua gumzo kubwa katika makanisa  mbalimbali  nchini.

Waumini wengi waliozungumza wamewashitukia baadhi ya viongozi hao  wa dini  kutokana na kile walichodai kuwa wamezidi kujilimbikizia mali huku wakiwahimiza (waumini) kutoa sadaka na michango mbalimbali ya mara kwa mara.

Kutokana na  hali hiyo,  baadhi ya waumini wamekuwa wakihama kutoka kanisa moja kwenda lingine huku wakiamini kuwa Mungu atawasaidia wabadilike kimaisha  au kumaliza matatizo yao.
Kutokana  na mgongano huo baina ya viongozi wa makanisa na waumini, baadhi ya wachungaji na maaskofu waliozungumza walikuwa  na michango yao juu ya hali hiyo na walizungumza kama ifuatavyo:
Askofu Mokiwa
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk. Valentino  Mokiwa  akizungumza na gazeti hili kuhusu suala hilo la viongozi wa dini kujitajirisha  alishauri kwamba  makanisa ya watu binafsi ambayo viongozi wao wamejipatia mali  nyingi  zenye utata wachunguzwe kwa karibu.

“Viongozi wa dini au muumini  kuwa tajiri  siyo jambo baya kwani hata sisi katika makanisa yetu ya Anglikana kuna maaskofu  matajiri na maskini na hakuna sheria  inayomkataza kiongozi wa dini kuwa tajiri  bali inategemea  jinsi alivyoupata, ambao haijulikani utajiri wao umetoka wapi, wachunguzwe,” alisema Askofu Mokiwa.

Aliongeza kuwa utajiri huo wa viongozi wa dini inabidi uwe ameupata kihalali, vinginevyo itakuwa ni dhambi kwa Mungu.
Alisema kwamba utajiri wa viongozi unaweza kutokana utafutaji kwa njia ya halali alitolea mfano wakati anasomea uchungaji nchini Marekani, kwamba   walikuwa wakifundishwa ujasiriamali wa kupata fedha kwa njia ya kilimo.

Mch. Mtikila
Naye Mchungaji Christopher Mtikila alisema kwamba viongozi wa dini kujitajirisha na kuwasahau waumini wao au kutumia fedha za waumini maskini  kujineemesha hao hawana wito wa Mungu.

Askofu Kakobe
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe alisema viongozi wa dini na hata wasio viongozi wanapaswa kujiwekea utajiri mbinguni na si duniani.

Askofu Kakobe ambaye amesifiwa na watu wengi kwa kuonesha kwenye televisheni nyumba na hata chumba chake cha kulala na kutajwa kuwa ni mfano, alisema kwake yeye anachokifanya ni kufundisha watu kuwekeza mbinguni.

“Siwezi kuacha kukemea watu wanaovaa vimini, wigi, kusuka nywele bandia, kuvuta sigara eti kwa sababu tutakosa sadaka,…kipaumbele ni Mungu,” alisema Askofu Kakobe.

Nabii Flora
Nabii Flora wa Kanisa la Maombezi lililoko Mbezi Beach kwa upande wake alisema  mtumishi wa Mungu aliye wa kweli hawezi kutajirika huku waumini wake wanalia na shida.

“Kanisa ni sehemu ya jamii ambayo inasaidia watu mbalimbali kupata Neno la Mungu pamoja na kusaidia shida za kijamii, si sehemu ya kiongozi kujitajirisha,” alisema.

Mch. Mtemela
Naye Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste jijini,  Alphonce Mtemela amesema kwamba katika Kitabu cha  Biblia Yohana 3.1 Mungu amesema utakuwa mbunifu kuwasaidia watu wako  unawaongoza ili wafurahie  wokovu wa Mungu.

“Kutokana na kifungu hicho ni wazi Mungu hataki mtu aishi  maisha ya majuto au masikitiko baada ya kumjua yeye.”
Akaongeza kwamba wokovu siyo mzigo ni furaha na kiongozi hapaswi kufurahi kuona watu anaowaongoza maisha yao yakiwa ni ya majuto wakati yeye anaishi  maisha mazuri.

Alisema watumishi wa Mungu waangalie jinsi ya kuwasaidia watu wenye shida na siyo waishie kubadili suti na kujitajirisha kila siku wakati waumini wanateseka  na kuishi maisha ya shida.

Mch. Rwakatare
Hata hivyo, Mchungaji Getruda Rwakatale kwa upande wake alipohojiwa hakupenda  kuchangia  lolote  kuhusiana na suala hilo.

Waumini wanasemaje
Baadhi ya waumini wa madhehebu kadhaa kwa nyakati tofauti walisema mtumishi wa Mungu wa kweli ni yule anayejali maisha ya waumini wake  na siyo yule anayejilimbikizia mali  huku ‘kondoo’ wake wakitaabika.

Mmoja wa waumini hao alisema anapeleka sadaka kanisani ambayo inamzidi uwezo, kitu ambacho si sahihi hata kwa Mungu.
Furaha Josephat ambaye amewahi kuwa muumini wa Kanisa la Efatha na sasa anasali Kanisa la Romani Katoliki, Mwenge amesema kwamba wachungaji  wanakosea wanapokuwa  matajiri.

“Haiwasaidii, ni bora mali zikiwa nyingi  zitolewe kwa wasiojiweza pamoja na yatima kama sadaka,” alishauri Josephat.
 Aliongeza kwamba  viongozi wengi wa dini wanapenda kujilimbikizia mali  bila kutoa  msaada, akawashauri waangalie  maeneo mbalimbali ya kutoa msaada kama vile kujenga hospitali, shule na visima vya maji.

 Naye Mary Andemile ambaye alijitambulisha kuwa huwa anasali Kanisa la Gwajima alisema kuwa viongozi wa dini wanapaswa wawasaidie  watu wenye hali duni badala ya kujitajirisha.
Alitoa mfano kuwa Mchungaji  Gwajima
ni kiongozi ambaye siyo tajiri lakini amekuwa akiwasaidia waumini  wake jinsi ya kujikwamua na maisha magumu.
Muumini mwingine, Francis Mbena  kwa upande wake aliwashauri viongozi wa dini wasiwafanye waumini wao kuwa  vyanzo vyao vya mapato ili wawe matajiri.

“Ni vema mtu akatoa sadaka kulingana na uwezo wake, wasitumie imani kuwalazimisha waumini kutoa michango mingi huku wakijua hali zao ni duni, huko ni kuwanyonya,” alisema.
 Daudi Antony kwa upande wake amesema kuwa ukweli ni kwamba kutokana na utajiri wa viongozi kuwa mkubwa, wakiwemo wanasiasa, taifa linaelekea kugawanyika.

“Makanisani, serikalini sasa hakuna huduma, baadhi ya wachungaji wamegeuza makanisa kama miradi yao vivyo hivyo kwa viongozi wa serikali, ofisi zao ni miradi ya kuchumia fedha au ni biashara,” alisema Anthony.

Naye Gerad Philipo amesema viongozi wengi wa dini wameshindwa kuwa na huruma kwa watu wanaowaongoza kwani huwakamua na hasa ile kanuni ya fungu la kumi, alidai inaumiza wale wasiokuwanacho.
Views: 1614
Tags: uwazi11


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...