Saturday, February 18, 2012

KANUMBA AFUNGUKA ALIVYOTESEKA: "Baba yangu alianza kunitafuta baada ya kuona nimepata mafanikio..."



STAA mkubwa katika tasnia ya filamu za Kibongo, Steven Kanumba Charles ‘The Great’ ameweka wazi siri za maisha yake ya utotoni na kumfumua baba yake mzazi aliyemwacha ateswe na mama wa kambo na kukataa kumsomesha...
Akizungumza kwa majonzi ndani ya Kipindi cha Take One, kinachorushwa na Runinga ya Clouds ya jijini Dar, Kanumba amemtupia zigo la lawama baba yake, Mzee Charles Kusekwa kwa kuchangia mateso yake.

“Maisha yangu ya utotoni yalikuwa ya mateso baada ya wazazi wangu kutengana, nilionja joto ya jiwe kwa kwenda kuishi kwa baba aliyekuwa ameoa mke mwingine, jambo hilo lilinikosesha furaha na amani ya utotoni,” alisema Kanumba.

Kanumba ambaye hadi sasa amejinyakulia umaarufu mkubwa kutokana na filamu zake, alisema wazazi wake walitengana akiwa anasoma darasa la nne.
“Nilikuwa naishi na mama, nilitamani sana kumjua baba yangu, nilimsumbua mama mpaka akanionesha baba yangu, nikaenda kuishi naye, nilikuwa nampenda sana baba yangu,” alisema Kanumba.

Akazidi kutupa madongo kupitia kipindi hicho kinachoongozwa na Zamarad Mketema kwamba, siku za mwanzo waliishi kwa furaha na baba yake pamoja na mama wa kambo lakini kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele ndipo kibao kilivyoanza kumgeukia.




Ukurasa wa mateso
“Nilianza kuamshwa na kutakiwa kuchota maji asubuhi na kwenda kufunga mbuzi kwenye malisho kisha niliporudi nilitakiwa kuosha vyombo.
“Nikitoka hapo, nilitakiwa kwenda shule, sisi tumesoma kipindi cha viboko, ukifika shule unakutana na mwalimu wa zamu, unachapwa bakora, mwalimu wa darasa naye anakupa adhabu kwa kuchelewa kipindi chake…,” alisema Kanumba na kuongeza;
“Unajua Shinyanga kuna shida kubwa sana ya maji, niliporudi nyumbani kutoka shuleni nilitakiwa kwenda kuchota tena maji. Nilipewa tolori na madumu sita ya kwenda kuchota maji.”
Staa huyo alisema kuwa baba yake alikuwa akiyajua mateso aliyokuwa akiyapata lakini hakuchukua hatua zozote ili kumnusuru.
“Kule Shinyanga huwa tunachimba mashimo ya taka, hakuna ‘ma-dastibin’ kama huku, siku moja mama alinitaka kuwapelekea mbuzi maganda ya viazi lakini kwa kuona kuwa mbuzi wale walikuwa wameshiba na ilikuwa usiku niliona bora niyatupe kwenye shimo la taka.
“Mama alipogundua nimefanya hivyo, hakujali kama ni usiku, akanitaka niingie shimoni na kuyatoa yale maganda na kuwapelekea mbuzi, niliingia kwenye shimo kukiwa na giza na kuanza kuyakusanya ingawa nilikuwa sioni kutokana na giza.
“Baba alipita, alidhani ni paka, kabla ya kurusha jiwe, aliwasha tochi na kuniona, aliniuliza nilikuwa nafanya nini, nikamweleza,” alisema Kanumba na kusema kuwa hiyo ilikuwa sababu tosha ya baba yake kuona mateso yake na kuweza kumnusuru.
Kanumba alisema mama yake mzazi, Flora alimchukua baada ya kusikia mateso aliyokuwa akiyapata.
“Mama akiwa anakwenda harusini na wenzake aliniona nikichunga mbuzi mchana wa jua kali. Alijisikia vibaya sana, akaamua kunisaidia bila ya aibu na akanichukua kabisa pale alipoyaona mateso yangu,” alisema Kanumba. 
Kanumba aliongeza kuwa alijitahidi sana kumshawishi mama yake awasiliane na mzazi mwenzake huyo ili wasaidiane kumsomesha.
Mama yake alimfikisha mzazi mwanzake huyo Ustawi wa Jamii, lakini siku ya mashauri, mama yake alirudi na hakutaka kumwambia Kanumba kilichotokea.
“Nilijitahidi kutaka kujua lakini mama aliniambia kuwa atanisomesha yeye mwenyewe, nilishindwa kuelewa lakini nikiwa nacheza nje nilimsikia mama kupitia dirishani alipokuwa akiongea na wanawake wenzake kwamba baba yangu amesema kuwa hawezi kumsomesha jambazi.
“Eti baba alisema kuwa nilikuwa nikimuibia mama yangu wa kambo fedha,” alisema Kanumba kwa majonzi.

Akiri kumpenda Mama kuliko Baba
Bila aibu wala simile, Kanumba alisema kuwa anakiri nafsi yake inampenda mama yake mzazi kuliko baba yake.
“Samahani sana najua hata baba anaweza kuwa anaangalia kipindi hiki lakini ukweli ni kwamba nampenda mama kuliko baba yangu,” alisema  kwa unyonge na kuongeza:
“Kusema kweli baba yangu alianza kunitafuta baada ya kuwa maarufu, lakini mimi nilishawasamehe yeye pamoja na mama yangu wa kambo, kwani hadi sasa huwa nawasiliana nao kwa simu, nawasaidia panapowezekana.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...