Wednesday, December 14, 2011

MAHABA: Kama hujampenda, usianzishe uhusiano naye!


Mungu ni mwema rafiki zangu, ametukutanisha tena katika ukurasa huu wa kuelimishana haya na yale
kuhusu maisha yetu ya kiuhusiano. Sina shaka umekuwa ukijifunza vitu
vipya kila siku kupitia safu hii. Naamini utakuwa katika uhusiano
thabiti usiotingishika baada ya kuelimika hapa...

Kuna wakati huwa najiuliza kwanini tunakuwa na wapenzi, kwanini mapenzi yakawepo? Kwanini tunaoa na kuolewa? Kwanini baadhi ya watu huamua kujinyonga baada ya kuachwa na wapenzi wao? Kwanini mapenzi yamekuwa sehemu ya maisha yetu?

Kwanini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Huwa najiuliza maswali mengi yenye kwanini, yakihusisha mapenzi. Kwa ujumla kama nilivyo na maswali mengi, majibu pia yamekuwa mengi.
Kwa vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Siyo tamaa ya mwili.

Mapenzi hayo, hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndio unayempenda utakuwa upo katika kifungo cha utumwa wa mapenzi. Kama ndivyo, kwanini uwe mtumwa?

Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi!
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako! Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe!

Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwanini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi dada zangu!

Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla. Hii inaama kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, na lazima utamkaribisha!

KUJILAZIMISHA KUPENDA!
Baadhi ya wasichana, akitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo. Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo.

“Pesa anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitajitahidi kumpenda taratibu,” baadhi ya wasichana huwaza hivi. 
Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa. Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba, wapo pia ambao ndoto zao huwa ni kufunga ndoa, haijalishi kama moyo wake utakuwa umeanguka kwa mtu huyo au lah, lakini kikubwa kwake ni ndoa.

“Acha niondoe hii nuksi, yaani muda wote huu siolewi? Tayari nina miaka 34 sasa, hii ni bahati, acha nikubali,” wapo wanaowaza hivi, mawazo ambayo si sahihi kabisa.

Ndugu zangu, ndoa ni ahadi, kama ni kweli unataka kuishi kwa amani katika maisha yako yaliyosalia hapa duniani, lazima ufanye uchaguzi sahihi wa mwenzi wa maisha yako. Ukifanya kosa hili tu, kila kitu kinakuwa kimeshaharibika. Kama ni safari ya mateso, wewe tayari utakuwa umeshakata tiketi.
Achana na mawazo ya kujifunza kupenda baada ya kuingia katika mapenzi, jambo hilo haliwezekani rafiki zangu, lazima useme na moyo wako, ambao ndiyo haswa unaotakiwa kusikilizwa na kupewa nafasi ya mwisho ya kuamua!

MADHARA YAKE...
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndio msingi wa maisha ya ndoa. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.

Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, siku hiyo lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo, na kama ana hasira, anaweza kukua. Yote hayo ya nini?
Inaelezwa wazi kwamba, kati ya sababu kubwa kabisa za wanandoa wanaosaliti ndoa zao, pamoja na tamaa, pia ni kukosa msisimko kwa mwenzi wako. Msisimko unakosekanaje? Pale unapohisi kwamba upo katika ndoa kwa kujilazimisha, kutimiza wajibu, lakini penzi la ndani huna.

BAKI NA HILI!
Kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza likaharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaeweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa.
Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo. 

Kwanini ulazimishe mapenzi? Kama humpendi, humpendi tu, acha hisia zizungumze zenyewe. Usilazimishe mambo yasiyowezekana ambayo mwisho wake utakwa mbaya zaidi kwako. Hili ni somo lenye mafunzo ya kutosha kwako rafiki yangu. Ahsante sana kwa kusoma.

No comments:

Post a Comment