Tuesday, September 6, 2011

POLISI WAPIGA STOP NDOA KANISANI..

JESHI la Polisi Mkoani Arusha limeisambaratisha ndoa ya nabii maarufu jijini humu, Hebron Kisamo wa Kanisa la Yesu ni Bwana na Mwokozi wa Mataifa Yote, iliyokuwa ifungwe kwa mbwembwe na mashamsham yote, Amani limeshiba data.

Tukio hilo la kuipangua ndoa lilijiri Agosti 27, mwaka huu ndani ya kanisa hilo lililopo Moshono nje kidogo ya Jiji la Arusha baada ya madai kwamba, bwanaharusi ana ndoa nyingine aliyofunga na Bi. Detiva Mathew Temba.





Siku ya tukio, Nabii Kisamo alikuwa afunge ndoa na Nancy Mdee ambaye ni  Mtangazaji wa Kituo cha Runinga cha KTN kilichopo  nchini Kenya.

Kuvunjwa kwa ibada hiyo ya ndoa muda mfupi kabla haijaanza kulifuatiwa na taarifa zilizovuja kuwa, nabii huyo ana mtoto mmoja na mke ambaye alifunga naye ndoa mwaka 2004  katika Kanisa la Calvary Temple (TAG) la jijini hapa.





Taarifa za uhakika zilieleza kwamba, nabii huyo alifanya maandalizi ya ndoa wakati mkewe akiwa safarini jijini Dar.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, wapambe walimtumia ujumbe kwa njia ya simu ya mkononi mke wa nabii huyo na kumtaarifu kuwepo kwa ndoa hiyo,mbaya zaidi muoaji huyo hakuwa amelipa mahari kama ilivyo ada na desturi za Kiafrika.





Baada ya kupata taarifa hizo, mke wa nabii huyo, alirejea haraka jijini Arusha akiwa na cheti cha ndoa kati yake na Nabii Hebron.

Hata hivyo, mpango mzima wa harusi hiyo unadaiwa kuratibiwa na mama mzazi wa bibiharusi bila kuhusishwa ndugu mwingine.

Habari zilisema kuwa, siku ya tukio, Dativa alilifikisha suala hilo upande wa ndugu wa bibiharusi mtarajiwa ambao walipigwa na butwaa na kuamua kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kabla ya muda wa ndoa hiyo kufungwa haujawadia.

Kwa mujibu wa mmoja wa wanandugu upande wa bibiharusi mtarajiwa, James Mdee alisema taarifa za kuolewa kwa mdogo wao hawakuwa wakizifahamu mpaka siku ya harusi walipoambiwa na mke halali, ndiyo maana waliamua kukimbilia polisi kutoa taarifa.

Nabii huyo, bibiharusi  na wapambe wao wawili, walikamatwa na kuhojiwa kwa zaidi ya  saa nne.
Mbele ya maafande, nabii huyo alikiri kuwa na mke na mtoto mmoja, lakini akasema ndoa yake hiyo haina amani kwa muda mrefu ndiyo maana aliamua kuoa mke mwingine.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Arusha, Zubeir Mwombeji alikiri kupokea malalamiko hayo na kuwahoji wahusika.
Hata hivyo, alisema tayari suala hilo limepatiwa ufumbuzi kwa kuzuia kufungwa kwa ndoa hiyo.

 Alisema kuwa, zoezi la kuipiga nyundo ndoa hiyo lilifanyika saa 11.30 jioni ambapo bibiharusi huyo alitinga kanisani akiwa amevaa ‘kininja’ ili asijulikane kwa sababu tayari walishasikia mambo yamefika polisi.

Mkuu huyo wa kituo aliongeza kwamba, polisi walifika ndani ya kanisa na kumchomoa yeye na wapambe wake wakiwa katikati ya watu na kuondoka naye.

Hali hiyo ilikatisha kwa muda maombi yaliyokuwa yakimwagwa kanisani hapo na nabii huyo huku waumini na wapambe waliokuwa wamefurika wakishangaa na kutoamini kilichotokea.

Ndani ya Ukumbi wa Ebeneza ambapo sherehe za harusi zingefanyika,  maandalizi yaliendelea huku wapambaji wakiwa hawana hili wala lile.

Habari zaidi zinapasha kwamba,maandalizi ya ndoa hiyo yaligharimu kiasi cha shilingi Milioni 10 ambapo baadhi ya waalikwa, waliofika na wengine walikacha baada ya kusikia mambo yaliyojiri.

Nabii Hebron alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia tukio hilo, hakuweza kupatikana licha ya kupigiwa mara kadhaa na kuita bila kupokelewa.

1 comment:

  1. baada ya kufanya uchunguzi na upembuzi wa kina, nimethibitisha yafuatayo.
    Huyo aliyekuwa akidai ni bibi harusi (Bi Dativa), alimwacha Hebron, akaenda kuolewa na kuishi na mwanaume mwingine, wakati huo akiwa amemfilisi na kumwacha Hebron, na alizaa mtoto (jina ninalihifadhi). Halafu akawa anataka kurudi kwa Hebron kwa nguvu, tena baada ya kuzaa nje. Hivi hata kama wewe ni mwanaume, ukaoa, halafu mke akakukacha na kwenda kuzaa na mwanaume mwingine, halafu akurudie na mtoto wa mwanamume mwingine, je utampokea. Kwa kweli hata biblia inasema ndoa na iheshimiwe na watu wote, lakini pakiwepo na uzinzi, ndoa ruksa kuvunjwa!. Hapa namtetea nabii hebron. Big up Kwa hiyo hapa Dativa alivunja mwenyewe asitake kutuchanganya hapa.

    ReplyDelete