Tuesday, September 6, 2011

BALAA FACEBOOK



KIJANA mmoja aliyejulikana kwa jina la Tibasima (pichani chini), mkazi wa Ukonga, Dar ameshikiliwa na Jeshi la Polisi Tanzania, Kanda Maalum ya Dar es Salaam kufuatia kunaswa akitumia majina ya Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan, Anita na Hawa Kikwete kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook...







Kwa mujibu wa chanzo makini, kijana huyo alikuwa akijiita Hawa Jakaya Kikwete na kujenga urafiki na watu mbalimbali waliomtembelea kwenye ukurasa wake huo huku akidai yeye ni mtoto wa JK anayeishi na mama wa kambo, Mbezi jijini Dar.

‘Hawa’ alizidi kuandika kuwa, ndugu zake (akina Ridhiwan) wamemkataa kwa sababu alizaliwa nje ya nchi, akakulia na kusomea huko, hivyo tangu  amerudi Bongo anaishi na mama huyo wa kambo ambaye naye amekuwa akimtesa.

Akizidi kutumia mtandao huo huku akiweka picha ya  msichana mwingine (picha ya kwanza juu) kwa lengo la kujifanya ndiye Hawa, Tibasima  aliomba watu wamsaidie fedha kwa kutumia mtandao wa simu za mkononi.

Wapo waliosoma kwa masikitiko makubwa ‘mateso’ yake na kumsaidia kiasi cha fedha walichoweza.

Aidha, katika kutafuta misaada zaidi, siku moja alimuomba kompyuta mpakato ‘laptop’ rafiki yake mmoja wa kike aliyejiunga naye (jina tunalihifadhi) ili akafanyie mtihani.

Rafiki huyo alimkubalia na kumtaka aende nyumbani kwake, Kwasokota Chang’ombe, Dar  akaichukue, lakini kijana huyo alidai hataweza kwenda kwa sababu ana matatizo, hivyo akamtuma ndugu yake aliyemtambulisha kwa jina la Ridhiwan Junior.

Habari zinadai kwamba,Ridhiwan Jr aliyefuata laptop hiyo ni yeye Tibasima ambaye mpaka wakati huo alikuwa akiendelea kujulikana kama Hawa Kikwete.

Chanzo chetu kiliendelea kudai kuwa, baada ya mhusika kusubiri kurudishiwa laptop yale bila mafanikio,aliamua kumtafuta mtoto wa kweli wa Rais Kikwete aitwaye Miraji na kumuuliza kama ana ndugu anayeitwa Hawa ambaye anaishi na mama wa kambo, Mbezi ambapo alikataa.

Habari zinadai kuwa, Miraji alisema hata yeye ameshasikia malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali kwamba, wamekuwa wakitapeliwa na kijana  huyo kwa kujifanya binti wa JK.

Inadaiwa kwamba, Miraji alimpeleka raia huyo kwenye ofisi za usalama wa taifa ambapo nao walianza zoezi la kumsaka kijana huyo.

Hatimaye, hivi karibuni katika Hoteli ya Lamada, Ilala Dar, Tibasima alitiwa mbaroni na maafisa usalama na kumpeleka Kituo cha Polisi, Msimbazi, jijini Dar kwa uchunguzi zaidi.

Inasemekana baada ya kumbana vilivyo, kijana huyo alikiri kuwatapeli watu mbalimbali na maafande walimshinikiza kwenda kwake ambapo walikuta vitu  alivyowatapeli watu wengine.

Uchunguzi zaidi ukaonesha kuwa, mbali na ishu ya laptop, Tibasima aliwahi kuwaambia watu wanaomtembelea kwenye Facebook kwamba, anataka kuanzisha NGO’s aliyoipa jina la Survive People na kwamba, baba yake (JK) amekubali kumsaidia.

Wengi walikubali kujiunga na kikundi hicho, wengine walimchangia  fedha ili kukiendeleza.

Kwa upande mwingine chanzo hicho kilisema kuwa baada ya kijana huyo kukamatwa mhusika alichukua laptop yake ikiwa salama salimini.

Akiongea hivi karibuni, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Suleiman Kova, alikiri kuwepo kwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutaka kumtaja jina kwa kuhofia kuvuruga upelelezi.

Kamanda Kova alisema kuwa, mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.

No comments:

Post a Comment