Thursday, September 22, 2011

FAMILIA YAANDAA MAZISHI YA GADDAFI...



MAMBO yameshageuka, tajiri mkubwa duniani kugeuka maskini, kiongozi wa heshima kuwa mkimbizi, hali ni tete kwa aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, kwani familia yake imekata tamaa ya kunusurika.

Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa hivi sasa familia ya Gaddafi inaandaa mazishi ya heshima ya kiongozi huyo, kwani kuna asilimia nyingi akajiua kabla ya kukamatwa.
Mke wa Gaddafi, Safia, alitorokea Algeria mwishoni mwa mwezi uliopita akiwa na watoto wake watatu, Aisha, Hannibal na Mohammed.

Habari zinasema kuwa baada ya kuwasili nchini humo, aliieleza serikali ya Algeria kuwa mambo ni magumu, bado Gaddafi anapambana lakini kama familia watamzika kwa heshima kwa sababu ni mtu mwema.

Safia alisema, wananchi wengi wa Libya wanamuunga mkono Gaddafi, kwa hiyo alitabiri kurejea madarakani lakini akatia shaka: “Mapinduzi siyo ya wana-Libya, kuna uvamizi unaoshinikiza kuipora Libya, watu nyuma ya uvamizi huo hawataki kumuona kiongozi halali (Gaddafi) akiwa hai.

“Naye (Gaddafi) hatakubali kukamatwa, bora kufa kuliko kuuawa kwa kudhalilishwa. Hata mwanangu Saif al-Islam anatafutwa. Ikitokea bahati mbaya, sisi kama familia tutakuwa tayari kwa mazishi ya heshima, hilo ni jukumu letu na wana-Libya wote wanaopenda utawala wa haki.”





GADDAFI YUKO WAPI?
Jumamosi iliyopita, Baraza la Taifa la Mpito la Libya, lilitangaza kuwa halijui mahali ambapo Gaddafi yupo.

Msemaji wa baraza hilo (serikali ya waasi), Kanali Ahmed Omar Bani Walid alisema kuwa hakuna taarifa yoyote kuhusu mahali alipo Gaddafi.

Mara ya mwisho, iliaminika Gaddafi yupo kwenye Kijiji cha Josh akilindwa na wanajeshi wanaomtii lakini baada ya waasi kukivamia na kufanya utekaji lakini hawakufanikiwa kumpata.

Zipo taarifa kuwa kiongozi huyo amejichimbia kwenye Milima ya Nafusa, huku habari nyingine zikieleza kuwa kiongozi huyo yupo nchini Zimbabwe siku nyingi zilizopita.

UTAJIRI WAPUKUTISHWA
Aisha Gaddafi ‘Ayyesha’ alitoa machozi baada ya kupata taarifa akiwa Algeria kuwa nyumba yake iliyopo Tripoli, ilivamiwa na waasi, milango ikafunguliwa na kila mmoja akachukua kitu kinachomfaa.

Habari zinasema kuwa waasi baada ya kuingia kwenye nyumba ya Aisha, mamia ya watu waliingia kwa zamu, wakaogolea kwenye bwawa la kifahari la binti huyo wa Gaddafi, wakavuruga samani zilizopo ikiwemo kukaa bila nidhamu kwenye sofa za dhahabu zilizopo sebuleni.
Nyumba ya kifahari ya Saif al-Islam iliyopo Tripoli, imevurugwa vibaya na sasa inashikiliwa na waasi.

Kabla ya hapo, Machi mwaka huu, kikundi kinachojiita Mapinduzi ya Udhalimu (Topple The Tyrants), kilivamia nyumba ya Saif al-Islam iliyopo London, England na kuiteka.
Kikundi hicho kilitoa msimamo kwamba hakitaiachia nyumba hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 26.

Vyanzo vinasema kuwa Gaddafi ana utajiri wa kati ya shilingi trilioni 45 na 51, huku akiwa amehifadhi zahabu Benki Kuu ya Libya, zenye thamani ya shilingi trilioni 16.
Imebainika kuwa Gaddafi anamiliki shilingi trilioni 32 ambazo amewekeza kwenye biashara ya vimiminika nchini Uingereza. Tayari serikali ya Uingereza imeshatangaza kufilisi mali zote hizo.

WATOTO WAKE WAKO WAPI?
Gaddafi, 69, alikuwa na watoto wanane, mkubwa ni Muhammad ambaye ni mtoto wake wa pekee kutoka kwa mtalaka wa ndoa yake ya kwanza, Fatiha al-Nuri. Inadaiwa kuwa alijisalimisha kwa waasi lakini wapiganaji wanaomtetea baba yake, walimteka na kumpeleka kusikojulikana.

Saif al-Islam, anasakwa siyo tu na waasi bali pia Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu (ICC). Hajulikani alipo, ingawa alishatanguliza tamko kuwa atapambana kuwamaliza waasi. Saadi ambaye alitikisa kwenye soka, akichezea mpaka klabu za Ulaya, naye hajulikani alipo.

Saadi, alishachezea Klabu za Alahly Tripoli, Libya pamoja na Perugia, Udinese na Sampdoria za Italia. Muttassim, inaelezwa yupo nje ya Libya lakini naye hajulikani alipo. Katika utawala wa baba yake, alikuwa mshauri wa kijeshi wa serikali.

Saif al-Arab, aliuawa mapema na mashambulizi ya Nato, wakati Khamis hajulikani alipo ingawa waasi wanatangaza wameshamuua. Milad Abuztaia na Hanna, hawajulikani walipo wakati Mohammed, Hannibal na Aisha wapo Algeria na mama yao.

GARI LAKE LA KIFAHARI LIPO WAPI?
Gaddafi anamiliki gari la kifahari ambalo dunia nzima hakuna, ilielezwa na wana usalama wake kwamba ndilo salama kuliko yote duniani.

Ndani ya nchi hiyo, gari hilo lilijulikana kwa jina la Libyan Rocket. Lina muundo wa kipekee na linatajwa kuwa ghali zaidi duniani.

ANAMILIKI HOTELI KUBWA DAR?
Zipo habari kuwa Gaddafi anamiliki hoteli yenye hadhi ya Nyota Tano, Dar es Salaam lakini umiliki wake hautaji jina lake moja kwa moja.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...