Saturday, May 19, 2012

MAHABA: Tafsiri nyingine ya wivu na faida zake




Hakuna shaka kwamba somo la wivu linagusa eneo kubwa kwenye mapenzi. Palipo na upendo wa dhati basi wivu upo, ila pale ambapo hausomeki ni ngumu kuwepo kwa sababu hakuna hisia.
Wivu ni maumivu au wasiwasi wa kihisia! Inawezekana mwanzoni, wivu kwako ilikuwa msamiati lakini baada ya kuanza uhusiano, ghafla unajikuta unazongwa na mateso ambayo hayaonekani. Yap, umemuona mpenzi wako anazungumza kwenye simu na hauelewi, hicho unachohisi moyoni ndiyo wivu!

Wivu ni nini hasa?
Ukifunua kamusi ya Kiswahili, inatafsiriwa kwamba ni hali au tabia ya mtu kusononeka au kukasirika pale ambapo anamuona mpenzi au rafiki yake ana uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine. Maana hii haitoshelezi!
Kuwa na kijicho au gere, uhasidi pia ni tafsiri nyingine za wivu. Hata hivyo, kwa kile ninachokijengea hoja hapa pamoja na upana wa neno lenyewe katika ulimwengu wa sasa, bado hazitoshi kutoa maana inayokusudiwa.
Wivu ni hisia zenye utandu wa hofu, zinazosababishwa na hali ya kudhani kuna ushindani wa kimaslahi katika suala zima la kimapenzi. Hisia hizo zinaweza kujumlisha na maumivu yanayotokana na wasiwasi wa kuhisi hakuna uaminifu kati yako na mwenzi wako.
Kuna aina tatu za wivu: Namba moja ni wivu wa mashindano. Hii hutokea pale ambapo kuna hali ya kushindana. Yaani kuna mtu mwingine anakuwa na lengo na mwenzi wako, hivyo unajitahidi kumbakiza kwenye himaya yako. Ukimuona naye moyo wako hautakuwa sawa.
Kuna wivu wa kusingizia. Hii inamaana kuwa unakuwa unamtuhumu mpenzi wako kwamba ana wivu kupindukia, wakati ni wewe mwenyewe ndiye unayesumbuliwa na wivu.
Aina ya tatu ni wivu wa kujidanganya kimawazo. Hapa unakuwa hauna imani na mpenzi wako, kwa hiyo ukikaa unakuwa na fikra kwamba mwenzio anakusaliti au anafanya yasiyopendeza, wakati hilo halipo.
Je, wivu ni mbaya kila siku?
Ni swali la kujiuliza katika somo la wivu. Jibu lake ni rahisi kwamba si kila mara ni mbaya. Wakati mwingine una faida zake na umewezesha uhusiano wa wengi kudumu.
Kitaalamu, inashauriwa kwamba kiasi fulani cha wivu ni muhimu kwenye mapenzi. Sayansi ya saikolojia inatoa muongozo kuwa hisia zako za wivu zinaweza kukusaidia kukulinda kwenye uhusiano wako.
Faida za wivu ni kama vile kuongeza kiwango cha mawasiliano. Mpenzi wako akiwa anakuonea wivu, atakuwa anakupigia simu mara kwa mara, hivyo kusaidia kuwaweka karibu.
Wivu husaidia kutoa tafsiri ya mipaka kwenye uhusiano, mpo pamoja, kwahiyo wanaowazunguka watajua kinachoendelea kati yenu, pia chochote kuhusu marafiki wa pembeni kitakuwa kina maelezo ya kutosha.
Wivu pia husaidia kuwafanya wahusika kutambua wajibu wao, hivyo kufanya uhusiano kuwa na afya zaidi.
Hata hivyo, kuwa na mpenzi (mume au mke) mwenye wivu inakuhitaji zaidi uwe muelewa kuliko kawaida, kwahiyo hapa chini kuna mambo ya kuzingatia. Ni ushauri kwako.

UVUMILIVU
Upo na mpenzi wako au pengine mmekwishafunga ndoa, ila tambua kwamba wivu unaweza kukufanya uwe na hasira kali dhidi ya mwenzi wako. Hiyo haiwezi kuwa sawa. Watu wanakua, wanabadilika na kupevuka.
Kitu ambacho kilikuwa muhimu wakati mnaanza uhusiano wenu, hakiwezi kuwa na msingi ule ule baadaye.
Ipo wazi kwamba ushirikiano kati ya watu wawili wanaopendana na kuamua kujenga maisha pamoja, unasaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa migogoro inayoweza kusababishwa na wivu.
Mshauri wa ndoa, Susie Moore katika makala yake yenye kichwa: “Me and My Husband” akiwa na maana ya mimi na mume wangu anaandika: “Hakika mimi huwa namwambia mume wangu kwamba simuonei wivu kwa sababu tunashirikiana kwa kila kitu, ananishirikisha na mimi nampa nafasi yake kama mume. Wivu utoke wapi?
“Hata hivyo, hii haikuja hivihivi, huko nyuma tulipita kwenye matatizo mengi. Kila saa nilimtilia shaka mume wangu, sikumuamini. Hata hivyo, nilimvumilia, nikagundua yupo sahihi kwangu. Tunashirikiana. Nawe ukimvumilia mumeo halafu mkawa mnashirikiana, wivu hauwezi kuwagombanisha.”

No comments:

Post a Comment