Friday, May 25, 2012

MAHABA: MPENZI WAKO AMEPOTEZA MSISIMKO KWAKO?




NAKUKARIBISHA kwa moyo wa upendo katika darasa hili. Nakuhakikishia hutajuta kupoteza muda wako, maana utavuna mengi. Wadau wa Let’s Talk About Love, kitu kinachoitwa matatizo katika uhusiano wao hakipo kabisa.
Karibu kwenye familia hii nawe uwe bora zaidi na zaidi kwa mwenzako.
Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, utakuwa mwalimu wa wengine. Rafiki zangu, katika mapenzi ni jambo la kawaida kabisa kugombana na kufikia hatua ya kutengana kwa muda.
Naomba hapa niweke wazi kitu kimoja, nazungumzia zaidi kwenye uhusiano wa mapenzi, kabla ya ndoa. Nazungumza na wachumba zaidi.Inawezekana kukawa kumetokea kutokuelewana baina yenu, mkaachana. Ukiwa nje ya uhusiano wako, ukagundua kwamba chanzo cha matatizo yote ni wewe.
Inategemea umemfanyia nini? Labda umemtukana sana, umeharibu samani zake nk, lakini mwisho wa siku unagundua kwamba wewe ni chanzo cha matatizo hayo ya kutengana. Kama kweli mna mapenzi ya dhati, mnaweza kukutana na kujadiliana pamoja, halafu mwisho wa siku mkajikuta mmeamua kurudiana.
Kinachowarudisha pamoja ni mapenzi ya dhati pekee na si kitu kingine chochote, lakini pamoja na penzi hilo, unatakiwa kufahamu kwamba mwenzako atakuwa na majeraha ndani ya moyo wake, atakuwa na vidonda ambavyo vinapaswa kuwekewa dawa ili apone kabisa. Mwenye wajibu wa kumwekea dawa ni wewe mwenyewe! Maneno yako makali, tabia zako mbaya, vituko vya kila aina na hasara ulizomsababishia, zinaweza kuwa sababu ya kumjeruhi moyo wake. Majeraha pia yanaweza kusababishwa na jinsi usivyo msikivu kwake, wakati akiwa anaamini kwamba wewe ndiye mpenzi wa maisha yake yote.
Sawa, ameamua kurudiana na wewe, kwa sababu anakupenda lakini bado anahisi kama utaendelea na matatizo yako ya zamani. Hakuamini. Anaona anaweza kuwa anatwanga maji kwenye kinu, ambapo ukweli ni kwamba mwishowe maji yote yatamwagika chini.
UTAMTAMBUAJE?
Yapo mengi, lakini kwa uchache sana, atapunguza mahaba na wewe. Ninaposema mahaba sina maana ya ngono, namaanisha mambo ya kimapenzi. Anakuwa mgumu kupokea simu yako, hata akipokea hazungumzi maneno ya kimahaba kama zamani.
Ukimwambia: “I love you dear,” yeye anaweza kukujibu kwa kifupi: “Ahsante,” tofauti na zamani ambapo alikuwa akikujibu kwa mahaba mazito: “I love you too my sweetie.” Meseji zako hajibu, hata kama akijibu, atakujibu kwa mkato sana. Anaonekana hana msisimko na wewe. atakuwa mzito hata kuachia tabasamu akizunguza na wewe, hakuamini sana. Hakufuatilii sana, mara nyingi anaonekana mwenye mawazo mengi akiwa na wewe. Hafurahii anapokuwa na wewe na hata uchangamfu wake unapungua.
Kikubwa hapo ni kwamba hana imani kama ni kweli umeamua kwa dhati kubadilika na kurudi kwake mzima-mzima! Moyo wake unaendelea kukiri ndani kwamba anakupenda, lakini anashindana na imani kwamba yawezekana usibadilike, anachohofia yeye ni wewe kurudia makosa yale yale! Kama ukiona dalili zote hizo ujue wazi kwamba bado ana wasiwasi na wewe, moyo wake umejeruhiwa. Kufahamu ni hatua ya kwanza, nzuri na muhimu sana kwako, kwani angalau sasa utakuwa unajua upo kwenye uhusiano na mtu wa aina gani, huku ukiwa makini katika kutafuta suluhisho la tatizo lenyewe.
BAINISHA TATIZO
Kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kufanya ni kuonesha kwamba umeshafahamu kwamba hakuamini na hana msisimko tena na wewe. Unatakiwa umfanye ajue kwamba unatambua kinachoendelea, lakini unakiri kwamba ni haki yake kufanya hivyo, maana ni kweli kwamba mkosaji ulikuwa ni wewe.
USIMLAUMU
Katika makosa makubwa ambayo hutakiwi kufanya ni pamoja na kumlaumu! Hutakiwi kabisa kumlaumu kwamba anakosea kufanya anavyofanya. Lakini kwa vitendo, unatakiwa kuanza kumbadilisha taratibu huku ukionesha kumhurumia kwa hali aliyokuwa nayo.
Si tatizo kubwa sana marafiki, lakini linahitaji subira wakati ukilishughulikia.
TUKUTANE WIKI IJAYO.

No comments:

Post a Comment