Tuesday, May 15, 2012

Bosi adaiwa kumuunguza kwa maji mtoto wa ‘hausi geli’





AMA kweli ubinadamu kazi na uchungu wa mwana aujuaye mzazi kwani imedaiwa mtoto Fahad Rajabu anayeishi Mtaa wa Mzizima, Kariakoo jijini Dar es Salaam ameunguzwa kikatili kwa maji ya moto na mama mmoja aliyetajwa kwa jina la Mama Yassir Said.

Habari zinasema mara baada ya Fahad (2) kuunguzwa alipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako anaendelea kupatiwa matibabu.

Mama anayedaiwa kumuunguza mtoto huyo imeelezwa kuwa ni bosi wa mama mzazi wa majeruhi, aitwaye Mwamini Hussein (19) anafanya kazi za ndani yaani ‘hausi geli’.

Jirani wa mtuhumiwa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alidai kuwa baada ya kusikia mtoto analia sana alikwenda haraka ndani ya nyumba hiyo na kumkuta Fahad akiwa amekalishwa ndani ya beseni lenye maji ya moto.

“Nilimtoa haraka na kumvua nguo ambapo niligundua alikuwa ameungua sehemu kubwa ya mwili wake,” alisema jirani huyo.

Aliongeza kuwa baada ya mzazi wa mtoto huyo kuwasili, majirani walimshauri akamfungulie kesi mama Yassir ndipo alikwenda Kituo cha Polisi Msimbazi na kufunguliwa jalada lenye Na MS/RB/5333 kosa la kujeruhi kwa moto kisha mtoto akapelekwa Hospitali ya Amana.

Baadhi ya majirani waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, walidai baada ya mama huyo kufanya unyama huo alisikika akisema kuwa alilipiza kisasi kwa kumchoma moto malaika huyo kwani alidai Mwamini naye aliwahi kumchoma mwanaye.

Shuhuda huyo alisema kuwa, kufuatia hali ya Fahad kuwa mbaya alihamishwa katika Hospitali ya Muhimbili ambapo amelazwa Wodi ya Watoto Walioungua (Buning Unit).

Mwamini alipohojiwa na mwandishi wa habari hii kuhusu tukio hilo, alikiri mwanae kuunguzwa na bosi wake. 

Juhudi za kumpata mtuhumiwa ziligonga mwamba baada ya kuambiwa ametoweka nyumbani kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Faustene Shilogile alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema bado halijamfikia na kuahidi kulifanyia kazi.

No comments:

Post a Comment