Sunday, May 13, 2012

Askofu atimuliwa kanisani



ASKOFU wa Kanisa la Cathedral of Joy International, John Komanya anadaiwa kutimuliwa na mmiliki wa jengo la kanisa hilo lililopo Kipawa, Dar... 

Mtoa habari wetu (jina limehifadhiwa) alisema Komanya alitimuliwa katika jengo hilo kwa madai ya utapeli.

Kanisa hilo lipo katika Jengo la Victoria Services Station, Barabara ya Nyerere jijini Dar na kwamba mtumishi huyo alianza kufanya njama za kutapeli ndipo mmiliki akagundua na kumtimua.

“Askofu Komanya alituma watu wapige picha jengo hilo na kupeleka benki akidai ni lake kwa lengo la kupewa mkopo, mwenyewe alipogundua, akamwandikia barua ya kumfukuza,” alisema mtoa habari wetu.

BLOG hii ilifanikiwa kupata nakala ya Komanya kutimuliwa eneo hilo iliyoandikwa Aprili 23, mwaka huu ikimtaka kuondoka Mei Mosi, 2012 na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Victoria Services Station Ltd, Harold Elisamehe.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia ukweli wa mambo hayo, Elisamehe alikiri kumtimua Komanya kwa madai hayo.

“Ni kweli nimemfukuza Komanya katika jengo langu. Unajua nilipata taarifa anapiga picha jengo langu, nilipofanya uchunguzi nikagundua alikuwa akifanya hivyo ili akachukue mkopo benki,” alisema Elisamehe.

Askofu Komanya alipotafutwa mapema mwanzoni mwa wiki hii,  alikiri kufukuzwa eneo hilo bila kufafanua chanzo cha madai hayo. “Tumepata eneo lingine Kinondoni, tunafanya mpango wa kuhamia huko.”

No comments:

Post a Comment