Saturday, April 14, 2012
FILAMU YA KANUMBA KUFA YANASWA
KIFO cha Steven Charles Kanumba ‘The Great’ kinazidi kuibua mapya kila kukicha ambapo tayari imebainika kuwa filamu aliyotengeneza na kuigiza hivi karibuni, imebeba maudhui ya kifo chake kwa asilimia 99...
Filamu hiyo aliyoitengeneza marehemu Kanumba mwenyewe ambayo bado haijaingia sokoni, mwanzoni ilikuwa inaitwa Love of Price lakini baadaye Kanumba aliibadilisha jina na kuiita Love & Power.
Kwa mujibu wa mwandishi wa muswada (script) wa filamu hiyo, Ally Yakuti, mazingira ya kifo cha Kanumba kwenye muvi hiyo yanafanana na kilichomtokea usiku wa kuamkia April 7, mwaka huu nyumbani kwake maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza jijini Dar.
STORI ILIVYO
Stori ya filamu hiyo inaonyesha kuwa Edwin (Kanumba) alitokea kumpenda mwanamke lakini kwa kuwa yeye alikuwa maskini, ‘demu’ huyo aliyetumia jina la Christina (Irene Paul) kwenye filamu hiyo alimkataa akidai kuwa hana hadhi.
Alisema kuwa wakati Edwin (Kanumba) anaendelea kumfuatilia, akasikia kuwa mwanamke huyo anaumwa na kupona kwake lazima ipatikane figo ya mtu mwingine ili awekewe.
Stori inaendelea kutiririka kuwa Edwin (Kanumba) anajitolea kutoa figo yake moja.
Muvi hiyo inaonesha kuwa baada ya kupona, Christina (Irene Paul) anagundua kuwa mwanaume ambaye hamtaki kwa sababu ya umaskini wake, ndiyo aliyenusuru maisha yake kwa kumtolea figo.
Stori inaendelea kuonesha kuwa katika hali hiyo, mwanamke huyo anakuwa hana jinsi hivyo anakubali kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na Edwin (Kanumba).
ASUKUMWA, AFA PAPOHAPO
Katika filamu hiyo kuna kipande kinaonesha kuwa baada ya wawili hao kuishi kwa muda mrefu katika hali ya umaskini, Christina (Irene Paul) anashindwa maisha hayo, anambwaga Edwin (Kanumba) na kuwa na mwanaume mwingine.
Muvi hiyo inaendelea kuonesha kwamba kwa kuwa Kanumba alimpenda mwanamke huyo, hakukubali aondoke na katika kumzuia, ndipo mwanamke huyo alipomsukuma na kujigonga ukutani kisha akadondoka na kufa papohapo.
DAKTARI HUYOHUYO
Katika hali ya kushangaza, stori ya muvi hiyo inaonesha kuwa daktari ambaye anaonekana akimpima Edwin (Kanumba) kwenye filamu hiyo anayejulikana kwa jina maarufu la Kidume ndiye huyohuyo aliyempima Kanumba alipodondoka na kufariki dunia kiukweli usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
ALIYEMPELEKA MOCHWARI
Msanii wa filamu za Kibongo, Idrisa Makupa ‘Kupa’ ambaye kwenye filamu hiyo anaonekana akishiriki kumpeleka Edwin (Kanumba) mochwari, ndiye huyohuyo aliyeshiriki zoezi kama hilo la kumpeleka Muhimbili huku akimfumba macho baada ya kufariki kiukweli.
IRENE PAUL ANASEMAJE?
Akizungumza na Ijumaa juu ya ishu hiyo, mwigizaji Irene Paul ambaye kwenye filamu hiyo alitumia jina la Christina akionekana akimsukuma Edwin (Kanumba) na kufariki, alisema kifo cha staa huyo kimekatisha ndoto zake kwani ndiye aliyemwingiza kwenye filamu hivyo aliposikia habari hiyo mbaya ya kufa, mbali na kuzimia amekuwa akihisi bado ni ndoto.
“Kweli kwenye ile filamu nilimfanyia Kanumba mambo yote ambayo yamekuja kuwa ya kweli,” alisema Irene Paul akiangua kilio.
MASWALI TETE
Baada ya kujiridhisha na matukio yote ya kwenye filamu na uhalisia wa kifo cha Kanumba ndipo yaliboibuka maswali tete kuwa, je, Kanumba alifahamu juu ya kifo chake kwani kila kitu kipo kwenye filamu hiyo? Au ni nini kilichokuwa kikimtuma kufanya matukio yaliyoashiria tukio hilo?
TUJIKUMBUSHE
Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake na kuzikwa Aprili 10 katika makaburi ya Kinondoni, Dar.
No comments:
Post a Comment