Madawa ya kulevya.
Aina ya magari yaliyokamatwa.
IGP Mwema.
Nabii Flora.
MORIS Charles anayejitambulisha kuwa ni askofu wa kanisa moja la kiroho jijini Dar es Salaam amedakwa na unga hivi karibu katika Kijiji cha Mchingambili, mkoani Lindi.
Vyanzo vya habari vimeeleza kwamba Charles ambaye wakati fulani hujitambulisha kwa jina la Yusuph Mohamed Lutengwe alidakwa nyakati za usiku Januari 11, mwaka huu akiwa katika gari lake aina ya Toyota Land Cruiser (namba zinaifadhiwa ).
Taarifa hizo zimedai kwamba kudakwa kwa mtu huyo kulifuatia habari zilizowafikia polisi mapema ambapo waliarifiwa na aina ya gari analotumia Charles kupokea ‘unga’ au dawa za kulevya aina ya Heroine kilo 210 zenye thamani ya shilingi bilioni 9.4.
MTEGO WA POLISI
Imeelezwa kwamba siku ya tukio polisi waliweka mtego baada ya kupata taarifa ya kiongozi huyo kuwa atakuja katika kijiji hicho na gari lake la kifahari, wakapewa namba na raia wema.
Habari zinasema ilipofika saa tano usiku waliliona gari kwa mbali na lilipowakaribia, walilisimamisha lakini inadaiwa kuna mtu alichomoka ndani ya gari hilo na kutokomea gizani.
Vyanzo hivyo vinadai kuwa jeshi la polisi halikumjua mtu huyo lakini baadaye wakaambiwa kuwa aliyekimbia ndiye huyo anayejiita Askofu Charles ambapo mtu mmoja aliyekuwa akiliendesha gari hilo alitiwa mbaroni.
Habari hizo zilieleza kwamba muda huo huo watu aliokuwa akiwapokea wakiwa na madawa walikamatwa na polisi wa kikosi kazi.
Waliokamatwa wametajwa kuwa ni pamoja na Ismail Adamu (28), Hamad Said (27), Morine Amatus (22) na Pendo Mohammed Chausi (67) ambaye ni mwenye nyumba yalipokamatwa madawa hayo. Tayari watu hao wamepandishwa kizimbani.
Habari zinasema polisi walimfuatilia askofu huyo na kugundua kuwa anaishi Mikocheni, jijini Dar es Salaam na wakafanikiwa kukamata mali nyingine ambazo ni magari mawili ya kifahari aina ya Porsche Cayenne na Jeep Wrangler.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa askofu huyo amefanikiwa kuwakimbia polisi na ametorokea nje ya nchi Januari 15, mwaka huu.
Vyanzo hivyo vya habari vimedai kwamba kiongozi huyo wa dini huwa ana hati mbili za kusafiria, moja anatumia jina la Kiislam na huitumia anapotembelea nchi za Kiislam na nyingine yenye jina la Kikristo.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa hata magari anayotumia, usajili wake una utata kwani tulipofuatilia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) anayedaiwa kumiliki gari hilo Toyota Land Cruiser lililokamatwa na polisi ni Rashida Abushir Jumanne na aliuziwa na huyo kiongozi Januari 16, mwaka huu.
Afisa mmoja wa TRA alisema mmiliki wa kwanza wa gari hilo ni Makame .O. Juma na kumbukumbu zao zinaonyesha kwamba Juni 9, 20011 aliliuza kwa kiongozi huyo anayejulikana pia kwa jina la Lutengwe.
UTATA WA GARI
Kinachoshangaza ni kwamba Lutengwe alikimbia nchini Januari 15, mwaka huu, iweje auze gari kwa Abushiri Januari 16, mwaka huu wakati gari hilo tangu likamatwe Januari 11, mwaka huu bado lipo polisi hadi sasa?
Hata hivyo, mwandishi wa habari hii akiwa TRA alipata namba ya simu ya Abushiri, alipopigiwa alipokea mtu ambaye alijitambulisha kuwa yupo Morogoro na alisema kwamba anamfahamu Abushiri ambaye anaishi Sinza jijini Dar es Salaam.
Kijana aliyepokea simu aliwasiliana na Abushiri alimpa namba ya mwandishi na akapiga simu. Katika mahojiano alikana kwamba yeye hana gari aina ya Toyota Land Cruiser na hajawahi kulimiliki, akadai inawezekana jina lake na namba yake ya simu inatumika vibaya na wahalifu.
Abushiri alipohojiwa zaidi na mwandishi sababu ya simu yake kumkabidhi mtu ambaye yuko Morogoro wakati yeye yupo Dar es Salaam alijitetea kuwa huyo ni mdogo wake, hivyo ameamua kumpa hiyo simu ili aitumie.
Uchunguzi umebaini kwamba hata baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa na madawa ya kulevya, simu zao zimegundulika kuwa waliosajiliwa ni marehemu waliokufa kati ya miaka miwili na mitatu na wengine walikuwa wakiishi Morogoro.
Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alipoulizwa kuhusu kiongozi huyo alisema kwamba hayupo tayari kulizungumzia suala hilo kwa vile bado linachunguzwa.
Hata hivyo, alikiri kwamba kuna mfanyabiashara mkubwa wa madawa ya kulevya aliyekimbilia nje ya chini na kwamba magari yake yanashikiliwa na jeshi la polisi.
VIONGOZI WA MAKANISA
Baadhi ya wachungaji wa makanisa waliozungumza na gazeti hili kufuatia kadhia hii ya dawa za kulevya nchini, wameitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara hiyo haramu.
John Said wa Kanisa la Victorious la Ubungo External amesema kwamba sasa imefikia muda wa serikali na jamii kwa ujumla kupiga vita biashara hiyo na wanaokamatwa na dawa wachukuliwe hatua kali haraka.
Nabii Flora Peter wa Kanisa la Huduma ya Maombezi lililopo Mbezi Beach, Dar es Salaam amesema kwamba wanaokamatwa na biashara hiyo wachukuliwe hatua mahakamani kwani wanaumiza nguvu kazi ya taifa kutokana na ukweli kwamba vijana wengi wanaangamia na dawa hizo.
Mchungaji Timoth Mwankenja alisema:
“Kunahitajika jitihada za pamoja kati ya raia na polisi ili kupambana na biashara hii haramu. Kanisa letu tumewahi kutoa elimu mitaani, kunahitajika ushirikiano katika vita hii. Kama kuna viongozi wa dini wanajihusisha wachukiliwe hatua kali.”
Mchungaji Alponce Mtemela wa Kanisa la Pentekoste lililopo Kawe, amesema kwamba dawa za kulevya ni janga la taifa kwani wanaohusika na biashara hiyo haramu ni matajiri na wanaweza kufanya chochote, hivyo ameiomba serikali kuchukua hatua kali.
Mwanzoni mwa mwaka jana jeshi la polisi kitengo cha dawa za kulevya lilimkamata Askofu wa Kanisa la Lord Choose Chaersimatic Revived, aliyejulikana kwa jina la Chidi Okechuku.
Okechuku alikamatwa maeneo ya Mbezi Beach katika nyumba aliyopanga na alikutwa na kilo 81 za Heroine na kwa sasa kesi yake ipo mahakama kuu.
No comments:
Post a Comment