Thursday, December 15, 2011

MAHABA: Kosa kubwa la wanawake wanapoanzisha uhusiano!





Asilimia kubwa ya watu wapo kwenye uhusiano wenye matatizo. Wawili walioamua kuingia kwenye safari moja ‘spesho’ hawana maelewano. Wakati huyu anaingia mwingine anatoka. Kila mmoja anaishi kwa hisia zenye machale dhidi ya mwenzake.

Hali kama hiyo inapotokea mara nyingi humuumiza mmoja lakini tafiti za sayansi ya saikolojia zinaeleza kuwa ikiwa wewe unaumia leo basi mwenzako aliumia juzi kutokana na vitendo vyako. Kama sivyo, basi ngoja matokeo ya mateso atakayoyapata kesho.

Si uchawi wala haifungamani na utabiri wa wanajimu, isipokuwa ni muongozo wa elimu ya saikolojia. Hisia hubadilika, inapotokea mtu akiwa kwenye penzi la kina kwa mwenzake ambaye haheshimu hisia zake, hali hiyo itakwenda mpaka anayependa atachoka.

Siri ndogo ni hii, huyu anayependa moyo wake huingia ganzi kwa sababu ya maumivu ya mara kwa mara. Ikiwa wewe unapenda, kitu kikubwa unachohitaji ni kupata mapokeo chanya kwa yule ambaye penzi lako limemdondokea, hali ikiwa hasi lazima ikutese.
Itakutesa lakini baada ya muda moyo utaingia ganzi, hapo hisia zako zitahama kutoka kwenye kupenda kuelekea katika chuki. Yaani utamchukia unayempenda kwa kuona anaudhulumu moyo wako. Uhusiano ukifikia hapa, dawa kubwa ni kuachana.

Katika pointi hii, tatizo kubwa lipo kwa wanawake. Ingawa siku hizi mambo yamebadilika, kwa upande wangu naendelea kusimamia ukweli kuwa mwanaume ndiye mtu ambaye hutumia muda wake kuanzisha uhusiano, japo wanawake nao hawakatazwi.

Watu wanaweza kugombana, wakawa hawaelewani lakini hawajui kosa ni lipi. Maudhi kidogo yanawapeleka mbali kumbe kinachowatesa ni maumivu ya wakati wa kuanzisha uhusiano. Mapozi, dharau, nyodo na mambo mengine kama hayo.

Kama nilivyotangulia kueleza hapo awali, tatizo kubwa lipo kwa wanawake kwa sababu wao ndiyo hutongozwa. Hutumia nafasi yao ya kufuatwa kama fimbo kwa wanaume. Hushindwa kuwapokea vizuri na matokeo yake kuharibu jambo jema ambalo lingeweza kutokea baadaye.

Mwanamke anapofuatwa huamua kuzichezea shere hisia za mtu aliyetokea mbele yake. Anapogundua mwanaume mwenyewe anachachawa kutokana na kuzidiwa na mapenzi makubwa dhidi yake hapo ndiyo kabisa. Anaweza kumgeuza mpira wa danadana.

Mbaya ni kwamba mtindo wa kumgeuza mpenzi wake kitenesi cha kudundadunda, unaweza usiishie wakati wa kuanzisha uhusiano. Huendelea hata kipindi ambacho tayari wawili wamekubaliana kuwa wapenzi. Hali hii huibua mateso ya moyo kwa anayependa.
Hushindwa kutafsiri hisia za mwenzake kama kweli anapenda. Moyo wake unakuwa wenye kudundadunda, anajaribu kumshirikisha mwenzake jinsi ambavyo anajisikia lakini anaambulia mapokeo hasi kwa sababu anayempenda haoneshi hisia zozote kwake.

Kosa kubwa ni kwamba wakati mmoja anapoumia, yule anayehusika na maumivu hayo inawezekana hajui au anajua lakini anapuuza kwa kujiona yeye ndiye mwenye bahati ya kupendwa mpaka mtu anachanganyikiwa. Hii ni sawa na kucheza kamari kwenye mapenzi.

Tambua hili kuwa huyu atachanyikiwa leo, atashindwa kulala kwa sababu ya kukufikiria. Atatoa machozi lakini mwisho atachoka na kuona yote anayofanya ni ujinga. Atabadilika! Baada ya hapo na hisia za mapenzi huhama, mtesaji atateseka!
Ni saikolojia! Huyu aliyekuwa anapendwa ambaye mara nyingi hutokea kwa wanawake, husoma mabadiliko ya mpenzi wake, kwamba hamsumbui kama ilivyokuwa zamani, halalamiki, kwa sababu kachoka na yote huona sawa. Hapa ndipo mateso huhama.

Aliyekuwa anapendwa hutaka kulazimisha mpenzi wake arudi kama zamani. Yaani aendeelee kumnyenyekea, wakati kwa aliyependa akaumizwa mpaka akakinai, humuona mwenzake ni mtu asiyefaa, katili wa mapenzi, hujenga chuki ya ndani kwa ndani hata kama hatoionesha.

Hisia atakazokuwa nazo huyu ambaye anataka mpenzi wake arudi kama zamani ni kuwa mwenzake amepata mtu mwingine ndiyo maana kabadilia, hilo litamtesa. Ataonesha mapenzi yote lakini itabaki ni ile hali ya mwenzako anatoka wewe ndiyo unaingia.
Wakati mwingine watu hawa huendelea kuishi kwa machale mpaka ndoa. Hili ndilo zao la ndoa zisizo na maelewano, wanandoa kutokupeana upendo wa 100%. Hasira za mara kwa mara kwa sababu ya kumbukumbu ya mateso ya nyuma.

SULUHISHO
Watu wanaweza kuanzisha uhusiano mzuri na wakaishi kwa upendo. Muhimu ni kuzingatia heshima kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kama unatongozwa, usibeze maneno ya anayekutamkia, yapime kisha toa uamuzi. Tabia ya umapepe ni sumu, hivyo usiioneshe mwanzoni.


Itaendelea...

No comments:

Post a Comment