Wednesday, December 28, 2011

2011 MWAKA WA TABU



Gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida zimekuwa kubwa sana katika  kipindi chote cha Sikukuu ya Krismasi hadi kuelekea Mwaka Mpya, hii inatokana na bei za bidhaa mbalimbali kupanda maradufu, hali iliyowafanya baadhi ya wananchi kusema kuwa 2011 ni mwaka wa tabu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa hali hiyo imetokana na mfumuko wa bei ambao umezidi kuongezeka kama taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyoonesha.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumuko wa bei kwa Julai mwaka huu (Bajeti ya mwaka wa Fedha 2011/2012 ilipokuwa inaanza) ulikuwa ni asilimia 13, hadi kufikia Novemba umefikia asilimia 19.2.
Tayari bei za vyakula katika masoko ya Mwenge, Kariakoo, Buguruni, Mahakama ya Ndizi, Tandika, Afrikasana, Mbagala, Tandale jijini Dar es Salaam zimekuwa juu kupita kiasi na kuwafanya wananchi kulalamikia hali hiyo.
Katika masoko hayo, bei za vyakula zimepanda sana, kwa mfano kwa kilo mchele (za zamani zikiwa kwenye mabano) unauzwa Sh. 2,000 (Sh.1500), Unga wa sembe unauzwa Sh.1,000 (Sh. 800), Nyama ya ng’ombe Sh. 7,000 (Sh.5,000), dagaa wa Kigoma sh. 19,000 hadi Sh. 20,000 (14,000) na mboga ya jamii ya kunde Sh. 1,900 (Sh. 1,300).
Aidha, kuku wa kienyeji waliokuwa wakiuzwa kati ya Sh.8,000 na 10,000, sasa wanauzwa kati ya Sh. 15,000 hadi 19,000.



Uchunguzi wetu umebaini kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu ambapo bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na samaki kwa takribani asilimia 40.
 Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadamu hasa (watoto) ambao  wanasisitizwa kula vyakula vyenye protini.
Akizungumzia mfumuko huo wa bei, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameandika katika mtandao wake kuwa, hii maana yake ni kwamba, bajeti ya serikali iliyopitishwa na bunge Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6, sawa na shilingi 780 bilioni zimeyeyuka katika kipindi cha miezi minne tu ya utekelezaji wake.
“Kutokana na kasi ya ukuaji wa mfumuko wa bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwishoni mwa mwaka wa bajeti, serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na kutoa huduma kwa zaidi ya robo ya bajeti yake,” amesema Zitto.
Aidha, Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 Julai, mwaka huu, umefikia asilimia 24.7 hadi kufikia Novemba 2011.
Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo kati ya Novemba 2010 na Novemba 2011.
Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kilekile kwa shilingi 12,500. Bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi  kikiwa kimebaki pale pale, hivyo mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida hasa wa kijijini ambaye mapato yake ni madogo.




Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi, kwani mafuta ya taa yamepanda kwa asilimia 71 kati ya Novemba mwaka 2010 na  Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35.
Wataalamu wa mazingira wanasema madhara ya hali hii ni makubwa mno kwa maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo, bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24.
Wachunguzi wa mambo ya uchumi wanasema mfumuko wa bei unawasukuma Watanzania wengi hasa walalahoi  kwenye dimbwi la umasikini uliotopea, unapunguza uwezo wa serikali kutoa huduma za jamii kupitia bajeti yake na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama vile miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja n.k.
Baadhi ya wachumi, akiwemo Dk. Ngali Maita waliliambia gazeti hili juzi (Jumapili) kuwa ili kuondoa tatizo sugu la sukari nchini, serikali iruhusu na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa bidhaa hiyo.
Kuhusu vyakula watu binafsi wahamasishwe katika kuzalisha mpunga katika mabonde makubwa na kuhimiza uzalishaji mashambani na fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.
Dk. Ngali alishauri vyakula vilivyolundikana katika mikoa ya Rukwa, Mbeya na Iringa vinunuliwe mara moja na serikali na kusambazwa katika mikoa yenye upungufu wa vyakula na iongeze kasi ya  kununua bidhaa hasa sukari kutoka nje na isimamie bei ili  kupunguza upungufu wa bidhaa (scarcity) katika masoko.
Dk. Ngali aliishauri serikali kutengeneza kiwanda cha gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira hapa nchini.
Alisema mfumuko wa bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kulinganisha bei ya bidhaa hiyo na diseli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta, hali ambayo inawaumiza walalahoi.
Alishauri sera ya matumizi ya serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima kama vile posho nono na badala yake fedha nyingi zielekezwe katika uwekezaji wa shughuli za umma.
“Matumizi mengine ya serikali yanaongeza fedha kwenye mzunguko ama kwa kuwalipa watu wachache posho mbalimbali n.k au kwa kununua bidhaa na huduma bila mpango, hivyo kusukuma bei kuwa juu kinyume na uhalisia wa soko na kuwafanya walalahoi kuumia,” alisema Dk. Ngali ambaye pia ni mwanasheria.
Alionya kuwa tusipochukua hatua za haraka tutazidisha mfumuko wa bei na kufikia kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (33%) na hivyo viwanda kushindwa kukopa kwenye mabenki, wazalishaji wadogo watashindwa kulipa mikopo yao kwenye taasisi za fedha na hivyo kufunga uzalishaji.
Kutokana na takwimu hizo, wananchi wengi wamesheherekea Sikukuu ya Krismasi kwa unyonge huku wenye nazo wakila raha.

No comments:

Post a Comment