Monday, November 21, 2011

MAHABA: Penzi lenu halina amani kisa, simu zenu za mkononi?



Ni wiki nyingine tunakutana tena kupitia safu hii ambayo kimsingi tunakumbushana na kuelimishana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi. Naamini wewe msomaji wangu umzima bukheri wa afya na uko tayari kabisa kupitishia macho kile ambacho nimekuandalia kwa siku hii ya leo.
Mara kwa mara nimekuwa nikiandika makala zinazohusu 
tatizo la simu za mkononi kwa wapenzi kwani limekuwa ni kama wimbo wa taifa sasa. 

Tumekuwa tukishuhudia wapenzi wakiachana, walio katika ndoa wakitengana na wengine kukorofishana kila mara huku baadhi wakibaki katika uhusiano wa mashaka, chanzo kikiwa ni simu za mkononi.
Aidha, nimekuwa nikipokea simu nyingi sana kutoka kwa watu mbalimbali wakielezea namna ambavyo chombo hiki cha mawasiliano kimekuwa kikisababisha mtafaruku kati yao na wapenzi wao.

“Sina amani kaka yangu, mimi na mpenzi wangu tumekuwa ni watu wa kugombana kila wakati kwa sababu ya simu yangu ya mkononi, mara nyingi anahisi namsaliti na kila ninapoongea na simu anadhani naongea na wanaume zangu, naumia sana hadi wakati mwingine kuona bora nisiwe na simu kwani inaweza kusababisha nikaachana na mpenzi wangu wakati bado nampenda,”anaeleza Maria wa Dodoma.
Kwa kweli simu za mkononi kwasasa zimekuwa ni sumu katika uhusiano na hii inatokana na baadhi ya watu wasiowaaminifu kuzitumia katika kuwasaliti wapenzi wao.

Nilichodhamiria kukiandika wiki hii ni jinsi unavyoweza kumfanya mpenzi wako asihisi kwamba unamsaliti kwa kutumia simu yako ya mkononi. Nikuhakikishie tu kwamba, kwa kuzingatia haya nitakayoandika na kama mpenzi wako ni mtu mwenye uelewa mkubwa, simu zenu za mkononi haziwezi kuwaletea matatizo.
Kwanza, kama kweli wewe ni muaminifu kwa mpenzi wako unatakiwa kujiamini kila unapokuwa karibu naye na wala usioneshe kujishtukia. Wapo ambao kila wanapokuwa na wapenzi wao, wakipata sms tu, watajificha ili wasome haraka kisha wafute. Wakipigiwa wakiwa na wapenzi wao kama hamjui anayempigia basi atakata na kuizima kabisa. 

Hivi unapofanya hivyo unataka mpenzi wako akufikirieje? Utamjengea mazingira gani ili akuamini na kutohisi kuwa kuna mshikaji mwingine anakuzingua ama una uhusiano naye wa kimapenzi kwa siri? 
Kimsingi kujishtukia kwako pale unapokuwa na mpenzi wako kunaweza kukuharibia. Ndiyo maana nasema, kama kweli unampenda huyo uliyenaye usiweke mazingira ya usiri kwenye simu yako. Wakati mwingine kuwa tayari kumjibu pale atakapokuuliza ni nani aliyekupigia simu au ujumbe huo unatoka kwa nani. Siyo kila mara atakuuliza lakini pale atakapokuuliza mjibu.

Pili, unatakiwa kutambua kuwa wewe ni mpenzi/ mke au mume wa mtu. Hivyo basi siyo busara kujirahisi na kumpa kila mtu tena wa jinsia nyingine namba yako ya mkononi. Itoe kwa watu muhimu ambao hata siku wakija kukupigia simu ukiwa na mpenzi wako iwe rahisi kujieleza. 
Unaweza kumkuta msichana anakutana na mvulana na anatongozwa, awali anakataa lakini mwisho anaombwa namba yake ya simu na anaitoa. Utamuelewa vipi msichana kama huyu? Huyu ndiye wale nataka sitaki kama hujui. 

Hivi wewe huelewi kwamba wanaume wengi siku hizi wakishapata namba ya simu tu wameshamaliza kazi? Nasema wameshamaliza kazi kwa sababu ni wataalam wa kutongoza kupitia kwenye simu.
Sasa siku mtu kama huyo akikutumia ujumbe wa kimapenzi na mpenzi wako akauona utamwelezaje? Hawezi kukuelewa.
Tatu,unatakiwa kuwa makini sana na watu wanaokutaka kimapenzi. Hawa hata usipowapa namba yako ya simu wanaweza kufanya juhudi za kuipata kupitia kwa watu wako wa karibu. Kwa maana hiyo basi, wanaokusumbua ni vyema ukamweleza mpenzi wako. 

Hiyo itakusaidia! Lakini kama jamaa anakuimbisha kila unapokutana naye kisha unanyamaza, siku mpenzi wako atakapokuja kuwakuta sijui utamueleza nini akuelewe! Itakuwa ngumu.
Hata wewe mwanaume kama kuna mwanamke anakushobokea, mpe taarifa laazizi wako kwamba unajua demu fulani ananisumbua. Kimsingi usimfiche mpenzi wako katika kila jambo kwani waswahili wanasema, mficha maradhi kifo kitakuja kumuumbua!

No comments:

Post a Comment