Sunday, November 6, 2011

MAHABA: Dalili 5 za mpenzi anayetoka na rafiki yako



KWANZA namshukuru Mungu kwa kunijaalia afya njema na kunifanya nimudu kutimiza majukumu yangu ya kila siku likiwemo hili la kufunguana juu ya masuala mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Mpenzi msomaji, katika maisha ya sasa kuna vijitabia ambavyo vimeibuka kiasi cha kuyafanya mapenzi kuwavuruga walio wengi.
Tumekuwa tukisikia habari za baadhi ya watu kutembea na watu wao wa karibu lakini pia suala la mtu kutembea na rafiki wa mpenzi wake si geni masikioni mwetu.

Juzi nilibahatika kuzungumza na dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Furaha Juma wa Morogoro. Katika maelezo yake anamlalamikia mume wake ambaye amekuwa kwenye uhusiano na shoga yake kwa muda mrefu bila yeye kujua.

Anasema: “Huu ni mwaka wa pili rafiki yangu wa karibu amekuwa akitembea na mume wangu. Kuna dalili za hapa na pale nilikua naziona ila sikuzitilia maanani, nikaona niwe mpole lakini hivi karibuni ndiyo nimeujua ukweli, nimeumia sana.”

Kwa maelezo ya dada huyu tunaweza kuona ni kwa jinsi gani rafiki yako unayemuamini anaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wako kwa muda mrefu bila wewe kujua.

Hili limekuwa likiwaliza wengi pale wanapokuja kubaini usaliti wa aina hiyo kwa kuwa ni bora usalitiwe na mtu mwengine lakini siyo rafiki yako wa damu.  Kwa kuzingatia hilo, wiki hii nimeona niwaandikie dalili tano za mpenzi anayetoka na rafiki yako.

Ni dalili zilizofanyiwa utafiti kiasi kwamba ukiziona hizi na nyinginezo ambazo siwezi kuziandika leo kutokana na ufinyu wa nafasi, utajua kuwa unasalitiwa, hivyo utatafuta mbinu za kukabiliana na tatizo hilo.

Simu, sms hazikauki
Unaweza ukakuta mara nyingi sana rafiki yako amekuwa akimpigia simu laazizi wako na wakati mwingine kumtumia sms za kufumba. Tena inawezekana spidi ya rafiki yako kumpigia mpenzi wako ikawa ni kubwa kuliko jinsi anavyokupigia wewe.

Mbaya zaidi mpenzi wako akipokea simu ya rafiki yako huyo unaweza kukuta anaondoka na kwenda kuongelea mbali au ikiingia sms yake anaifuta fasta, hujiulizi kwa nini? Tena iweje ampigie mpenzi wako simu amsalimie tu wakati wewe ana siku mbili hajakutumia hata sms? Akili kichwani mwako.

 ‘Wanakutanaga’ bila wewe kujua
Kiutaratibu mpenzi wako anapokwenda kukutana na mtu tena wa jinsi tofauti maeneo flani ‘hatarishi’ ni lazima akuombe ruhusu kama siyo kukupa taarifa.

Sasa unaweza kushangaa siku unaambiwa mpenzi wako na besti wako walikuwa baa flani wakipiga stori, ukimuuliza mpenzi wako anakataa. Hii moja kwa moja inaashiria kuwa unazungukwa.

Urafiki unapungua
Mapenzi ni kitu cha ajabu sana. Huyo rafiki yako akishanogewa na penzi la mpenzi wako anaweza kufikia hatua ya kukuchukia bila sababu. Eti anaona kama vile unamuingilia anga zake.

Kwa maana hiyo ukiona rafiki yako amekubadilikia ghafla, tambua siyo bure, anakuchukulia wewe kama mke/mume mwenza.

Kupondwa kiaina
Usishangae pia rafiki yako akaanza katabia ka’ kumponda mpenzi wako na wakati mwingine kukushauri muachane. Kiukweli rafiki ambaye alikuwa akiufagilia uhusiano wenu halafu ghafla akaanza kuonesha kumponda ‘mtu’ wako, ujue ana lake jambo. Anachotaka muachane ili yeye ajilie vyake kwa kujinafasi.

Mapenzi kupungua
Ukishaona yote hayo hapo juu kisha ukabaini kupungua kwa mapenzi kutoka kwa mtu uliyetokea kumpenda, elewa unasalitiwa.
Hapo sasa hutakiwi kukurupuka wala kuchanganyikiwa, unachotakiwa kufanya ni kutulia na kufanya utafiti ili kubaini ukweli.

Nasema unatakiwa kutulia kwa sababu niliyoeleza hapo juu siyo ushahidi kamili kuwa mpenzi wako anatoka na rafiki yako.
Kitakachokusaidia ni kuanza kuwafuatilia nyendo zao kwa karibu na utaujua ukweli, baada ya hapo fanya uamuzi sahihi.

No comments:

Post a Comment