Mimi niko freshi kabisa na leo nataka kuzungumzia mada inayohusu penzi la siri na madhara yake. Kilichonisukuma kuandika juu ya mada hii ni kutokana mazungumzo niliyoyafanya na mmoja wa wasomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina la Alex mkazi wa Arusha akieleza namna alivyoingia katika aina hii ya penzi na kile kilichompata baadaye.
“Niliingia katika uhusiano na binti mmoja baada ya kutokea kumpenda sana ambaye tulikuwa tunafanya kazi sehemu moja. Katika maisha yetu ya kimapenzi akawa amenieleza kuwa, wazazi wake ni watu wa dini sana na hawataki kusikia kwamba ana uhusiano na mwanaume yeyote.
Akanieleza kwamba, pale kazini kuna watu wanawajua vizuri wazazi wake hivyo kama nampenda na nataka kuwa naye, nikubali penzi letu liwe la siri, yaani watu wasijue kama sisi ni wapenzi.
Maelezo yake hayakuniingia akilini kwani sikuwa na lengo la kumchezea bali ilikuwa tuanzishe uhusiano kisha baada ya muda nimuoe kabisa.
Kwakuwa sikuwa tayari kumkosa, nikaona nikubaliane naye kwanza huku nikiwa na lengo la kuja kumueleza baadaye kwamba, hakuna haja ya kuficha kwani sikuwa na nia mbaya.
Tukawa tunaendelea na uhusiano wetu kwa siri, siku moja nikashitushwa na tetesi kuwa, kuna mwanaume mmoja pale kazini kagombana na mwanaume mwenzake baada ya kubaini kuwa, wanashea penzi na demu mmoja ambaye ni yule aliyenikubalia tuwe wapenzi lakini kwa siri. Nilishangaa sana na sikuweza kuziamini tetesi hizo.
Nilijaribu kumuuliza lakini alikataa katakata huku akieleza kuwa, watu wanazusha tu. Kweli hakukuwa na mazingira yoyote yanayoonesha kuwa yule msichana alikuwa na mwanaume pale kazini lakini machale yakazinicheza.
Nikaanza kumuwekea mitego mbalimbali na siku moja nikagundua kuwa, kumbe yule binti hakuwa ametulia, ni kicheche ile mbaya. Amekuwa na katabia ka’ kuanzisha uhusiano na wanaume tofauti kwa siri. Nilichokifanya ni kuachana naye.”
Hayo ndiyo maelezo ya Alex ambaye alinisukuma kuandika mada hii ya leo yenye kichwa cha habari, penzi la siri na madhara yake.
Kabla sijaendelea, wewe msomaji wangu utakuwa umegundua kuwa, mtu yeyote anayekuambia penzi lenu liwe la siri ni lazima kuna kitu flani anataka kukificha.
Yawezekana ikawa kweli kuna sababu za msingi ambazo zinamsukuma kuwa katika penzi la sampuli hiyo lakini wengi ni matapeli tu.
Wapo watu wengi huko mtaani ambao wako katika penzi la siri na wengi ni wale waliooa au walioolewa. Unakuta mwanamke ameolewa lakini kutokana na tamaa zake anaanzisha uhusiano na mwanaume mwingine nje ya ndoa na kumuomba iwe siri kwani bado anampenda mumewe.
Na kweli wapo wanaofanikiwa kuishi kwa muda mrefu wakiwatumikia waume zao lakini pia wakiwatumikia wanaume nje ya ndoa kwa siri. Vivyo hivyo, waume za watu ni miongoni mwa wanaoanzisha uhusiano wa kimapenzi wa siri na aidha wake za watu au wasichana ambao hawakuolewa.
Ukiachilia mbali hao walio katika ndoa, cha ajabu sasa unakuta mtu hajaolewa/hajaoa anaingia katika uhusiano na mtu lakini anadai kuwa, penzi lao liwe la siri.
Hapo ndipo kwenye walakini. Hapo juu tumeona kwamba, wanandoa wanaingia katika uhusiano nje ya ndoa na kutaka iwe siri kulinda ndoa zao, je wewe ambaye uko ‘singo’ na unataka mtu wa kuwa naye maishani mwako, umepata lakini unataka penzi lenu liwe la kuibia, why? Kwanini?
Ninachokiona hapa ni kwamba, mtu anayeng’ang’ania kutaka penzi lenu liwe la siri atakuwa ni tapeli na inawezekana ama kaolewa, kaoa au ana mpenzi wake na tamaa zake ndizo zinamsukuma kuanzisha uhusiano na wewe. Huyu ni mtu ambaye unatakiwa kuachana naye mara moja kwani hawezi kuwa na ‘future’ na wewe.
Siku zote kwenye penzi la kweli hakuna usiri, usiri wa nini sasa? Wewe uko ‘singo’ na unataka uwe na mimi kisha unataka watu wasijue kuwa sisi ni wapenzi, kwanini nisihisi kuwa kuna kitu unataka kunificha?
Usikose kufuatilia sehemu ya pili ya makala haya ili uweze kuona madhara ya kuingia katika penzi la siri.
No comments:
Post a Comment