Sunday, October 23, 2011

MAHABA: Kumpata uliyemkusudia ni bahati nasibu...


Kama ilivyo ada leo hii tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba, nina imani kila mtu ana hamu kujua nimeawaandalia mambo gani.
Leo nilitaka tuzungumzie maisha ya mapenzi na kwa nini nimesema, kumpata uliyemkusudia ni bahati nasibu.
Mtakubaliana nami kuwa siyo wote wamepata kile walichokikusudia, nikiwa na maana gani? Kila mtu huwa na matamanio yake katika maisha au apate mpenzi wa aina gani ambaye ndiye chaguo la moyo wake.

Lakini wengi wameangukia kwenye mapenzi ambayo hawakuyaota katika maisha yao, ili kumpata mpenzi aliye bora kuna vitu ambavyo kila mmoja huviitaji. Kama sura na umbile zuri na kikubwa ni tabia nzuri.
Lakini wengi tumejikuta tukipata kimoja kati ya hivyo, nacho ni maumbile ya nje yenye siri kubwa ndani. Wapo waliopata wapenzi ambao huamini ndio chaguo la mioyo yao lakini hujikuta wakijutia uchaguzi wao.

Ni ukweli uliowazi kila mtu huangalia sana mtu alivyo kama sura umbile na umaridadi wake. Mtakubaliana nami kuwa kila mmoja huvutiwa na mwenzake kwa kumuangalia na kuvutwa kama sumaku.
Hata mnapoanza uhusiano wenu kila mmoja huwa na tumaini kupata mpenzi wa kweli mwenye mapenzi ya dhati. Ndiyo maana nikasema ni bahati nasibu kwa vile pale ni sawa na kufunua karata yako ambayo tayari unayo. Hapo kuna mambo mawili ule au uliwe.

Ukila utakuwa umepata kile ulichokikusudia kumpata yule uliyemkusudia. Lakini ukiliwa ujue karata uliyofunua siyo. Hapa ndipo watu huanza kujiuliza mbona mpenzi wangu au mwenzangu simwelewi, alivyomfikilia na jinsi alivyo, siyo kabisa.
Ni kwa nini?
Ni vigumu kuijua tabia ya mtu mara moja, wapo wenye tabia mbaya ya asili ambayo hujitahidi kuishi kutokana na mafundisho aliyoyapata ya uhusiano. Kwa vile aliishi kwa kufuata maelekezo na si asili yake lazima atarudia asili yake na kukufanya ujiulize ni kweli huyu ndiye yule niliyemuona na kutamani awe mpenzi wangu.

Kibaya zaidi tayari umeshajitia kitanzi hivyo huna jinsi ni kuvumilia huku ukitafuta msaada nje ya uhusiano ambayo si tiba kamili kama kumeza dawa za maumivu na tatizo hujirudia kwa vile ni ugonjwa.
Siyo wote ambao matatizo yao huwa hayapati ufumbuzi, nina imani kila aliye mcha Mungu huongozwa na muongozo wa maisha ya kuujua umuhimu wake ndani ya uhusiano na kujirudi.

Lakini wapo ambao uolewa au kuoa watu wasio wajua lakini nyumba zao hujaa upendo kuliko zile ambazo zilitumia muda mwingi kuchunguza tabia za huyo anayeoa au kuolewa.
Hapo lazima ukubali ndoa au kumpata mpenzi wa kweli ni habati nasibu hakuna mwenye uhakika wa asilimia 100. Napenda kuwauliza kitu kimoja, Je, ni kweli wazee wetu walikuwa na ujuzi wa kumjua mpenzi wa kweli?
Jibu na sema si kweli bali mafunzo ya wazazi kabla ya ndoa na nidhamu ya mwanamke ndiyo iliyolinda ndoa nyingi, hata kama uliyemuoa au kuolewa naye humpendi kwa vile wazazi wamempenda basi utaishi naye.

Siri kubwa ilikuwa wazazi kuzisimamia ndoa za watoto wao kuhakikisha zinadumu na uvumilivu na usiri ndiyo njia pekee ya kuokoa ndoa. Za sasa hivi ambazo nyingi zina kwenda na wakati miaka kumi wapenzi ishirini watoto kumi na kila mtoto ana mzazi wake.
Namalizia kwa kusema hata kama hukumpata yule uliyemkusudia, lakini ameisha kuwa wako jengeni tabia ya kutatua matatizo yenu ninyi wenyewe na matatizo yenu ya ndani yawe siri yenu.

No comments:

Post a Comment