Friday, September 9, 2011

Usifanye chochote mpaka ujue mambo yafuatayo...

Mara nyingi nimezungumzia umuhimu wa mtu kuwa makini katika kuchagua vitu anavyotaka kuvifanya kwenye maisha yake. Shabaha yangu ni kutaka kufundisha juu ya kuhakikisha jambo kabla ya kulitenda kwa sababu matendo wakati mwingine huambatana na majuto.

Sote tunafahamu kupitia jamaa zetu kwamba, wengi wao wanajuta kuoa au kuolewa, wanajutia pia kazi na biashara wanazofanya ambazo msingi wake mkubwa ni maamuzi.
“Najuta kuacha shule, ningejua mapema kwamba nitateseka hivi nisingeacha.”
Ukipekua ukurasa wa kila mtu anayejuta kufanya jambo lolote, utakuta mwanzo wake kulikuwa na maamuzi na wakati mwingine yaliambatana na msimamo.

Tukitaka kujifunza zaidi ni bora kila mtu akarejea maamuzi yake na hasa yale aliyofanya kwa furaha na kujikuta akivuna machungu na kujutia alichofanya.
Hapo tutabaini kasoro kubwa ya wanadamu wengi ni kuhakiki wanachofanya. Inaweza kuwa vigumu kukwepa mikwamo na majuto ya maamuzi kwa tafsiri fupi lakini kitaalamu kuna kinga ambayo kila mtu anatakiwa kuipata, nayo si nyingine, bali kupata elimu kabla ya kufanya jambo lolote.

Lengo la mwongozo huu ni kupunguza majuto na hasa ukizingatia kwamba karibu kila anachofanya mwanadamu kinaambatana  na hiyari yake. Sote tunafahamu kuwa dunia tunayoishi ina vitu vingi vinavyotutaka tufike kwenye hatua ya kuchagua kufanya au kutofanya.

Katika hali ya kawaida kutenda jambo si kitu kibaya, ni vema tukajifunza tu jinsi ya kufanya vitu sahihi.

KWANZA: Kabla ya kuamua kufanya kitu chochote, lazima mtu ajielimishe vya kutosha kuhusu jambo analotaka kulifanya. Ikiwa unataka kufanya biashara, kusoma au kufanya kazi, hakikisha kwamba unapata habari za kutosha kukufanya ufikie uamuzi wa uhakika. Kamwe usifanye kitu usichokijua kwa undani.

PILI: Inawezekana katika uhakiki wa wazo kabla ya matendo kukawepo na vikwazo ambavyo vinaweza kuweka zuio lisilokuwa na majuto isipokuwa kufikia hiyari inayoambatana na nia ya kupambana na changamoto. Si wakati wote mtu anaweza kuhakiki jambo kisha kuliacha kwa sababu tu amepata ugumu au kasoro fulani za kutenda, lahasha!

Kwenye hatua hii ya pili ni muhimu mtu kujiangalia mwenyewe na kukusanya ubunifu wa kusaidia kukwepa vikwazo. Kutafuta sababu ya uhakika kwa nini ameamua kufanya jambo fulani licha ya kuwepo kwa ugumu. “Kazi hii itakuwa ngumu lakini nitajitahidi kuifanya usiku na mchana ili kuimaliza.”

Majibu haya ya mikwamo husaidia sana kutia nguvu za kukabili ushindani ambao huleta mikwamo na hatimaye majuto.

TATU: Ni bora kupima faida na hasara ya kila unachotaka kukifanya kabla ya kuanza kukitenda. Ikiwa umeamua kuacha shule, jiulize kwanza faida na hasara yake ni nini? Ukijua itakusaidia sana.

Nakumbuka mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe aliacha shule na kwenda kufanya muziki ambao baadaye ulimletea mafanikio.  Alihakiki faida na hasara kwanza, na wewe fanya hivyo ili usijutie uamuzi wako.

NNE: Jiamini mwenyewe. Wakati mwingine binadamu wenzetu wanaweza kutuvunja moyo kwenye hatua ya kwanza ya kufikia maamuzi yaani kutupa taarifa potofu zenye kuogopesha. Jambo kubwa ni mtu mwenyewe kujiamini kwamba anachotaka kufanya atakiweza kwa hali yoyote na iwe mwiko kwake kushindwa.

TANO: Kutii kanuni za utekelezaji. Kuna wengine wanaweza kuamua kufanya jambo kinyume na kanuni zake. Utakuta mtu anaamua kulima kiangazi, pasipokuwa na rutuba au kutofuata muongozo wa kiasili. Si ajabu ukakuta mtu anaoa lakini akachagua kufanya mapenzi na mkewe kinyume na maumbile! 

No comments:

Post a Comment