Monday, September 12, 2011

MELI YA SPICE ISLANDERS YAZAMA PWANI YA NUNGWI IKIELEKEA PEMBA

Mv Spice ikiwa imezama pwani ya Nungwi....

MELI ya Spice Islander imezama usiku wa kuamkia leo ikiwa safarini kuelekea Pemba ikitokea bandari ya Malindi Unguja.
Meli hiyo inasemekana ilikuwa na abiria wapatao 610 ambapo juhudi za kuokoa majeruhi wa ajali hiyo zinaendelea hivi sasa.
Akizungumzia ajali hiyo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi amesema tukio hilo limetokea saa 8:30 za usiku.
Haji Ussi amesema meli hiyo iliondoka katika Bandari ya Malindi Unguja ikiwa katika hali ya uzima, lakini katikati ya safari ikapata hitilafu na kusababisha kubinuka na hatimaye kuzama kabisa.
Hadi sasa haijaweza kufahamika idadi kamili ya watu waliofariki, lakini vyombo vya uokozi vimefika katika eneo la tukio kutoa msaada.
Naibu Waziri Issa amesema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usafiri vya binafsi kama boti ziendazo kasi vimekwenda eneo la tukio kutoa msaada. Jeshi la Polisi Tanzania limetuma Helikopta yake kwenye eneo la tukio.
Awali, amesema Mamlaka zinazohusika zilipata taarifa za kuzama kwa meli hiyo baada ya Meli ya Mv Jitihada inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuripoti kuzama kwa meli ya Spice Islanders ambayo ililazimika kukatisha safari yake kuelekea Kisiwani Pemba na kwenda kwenye tukio. Serikali imesema taarifa zaidi zitakuwa zikitolewa na wananchi wameombwa kuwa watulivu.

No comments:

Post a Comment