Sunday, September 25, 2011

Jinsi ya kuishi na wafanyakazi wenzako

NAMSHUKURU Mungu kwa rehema na fadhila zake katika maisha yangu kwani amekuwa ngao na nguzo yangu kuu.

Ahsanteni sana wadau na wasomaji wa kona hii ya Jitambue kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkiuonesha kwani napokea simu nyingi za ushuhuda wa kujikomboa baada ya kusoma makala mbalimbali za kona hii.

Leo nimeona ni vyema tujikumbushe jinsi ya kuishi na wafanyakazi wenzetu katika Nyanja na ngazi tofauti. Kumekuwa na tatizo kubwa kwa baadhi ya watu namna ya kuishi na wafanyakazi wenzao hasa katika ofisi kubwa zinazojumuisha watu wengi.

Kabla ya kutoa dondoo za jinsi ya kuishi vizuri na wafanyakazi wenzako, naomba nitoe ufafanuzi mfupi ambao utakusaidia kukabiliana na vikwazo vya hapa na pale katika kuishi na watu wa rika mbalimbali katika jamii.

Kwanza ifahamike kuwa, popote palipo na mkusanyiko wa watu wengi, basi kuna mrundikano wa tabia, mila na desturi tofauti. Yaani kila mtu ametoka katika familia yenye malezi tofauti na ya kwao hivyo katika utofauti wa mambo hayo, ni lazima kutakuwepo na migongano ya hapa na pale kwani kila mmoja ana amini alichojifunza nyumabani kwao.

Hivyo basi, unapokuwa ofisini unakutana na watu wa aina hiyo. Watu ambao mnatofautina mambo mengi ikiwemo uelewa, vipaji na ustaarabu.
Hivi ndivyo unapaswa kuishi na wafanyakazi wenzako:

Soma Mazingira
Unapokuwa ofisini na wafanyakazi wenzako, jitahidi sana kusoma mazingira ili ujue ni mambo gani hayatakiwi na ni yapi yanatakiwa kufanyika na kwa wakati gani. Hii itakusaidia kuepuka baadhi ya migogoro na wafanyakazi wenzako.

Ninaposema kusoma mazingira ninamaanisha kuwa, kuna baadhi ya mazingira ndani ya ofisi ambapo watu hawapendi kuchangia vifaa kama kompyuta na vingine. Sasa unapoingia na utaratibu wako pasipo kusoma na kuyajua mazingira hayo, unajikuta moja kwa moja unavunja taratibu za kiofisi kwa sababu tu hukusoma mazingiara tangu awali.

Tambua udhaifu na uimara wa wafanyakazi wenzako:
Kila binadamu ana udhaifu na uimara wake. Katika mazingira unayofanyia kazi, jitahidi sana kumsoma kila mfanyakazi mwenzako ili ujue ni kwa namna gani utaweza kuishi naye.
Kuna baadhi ya watu hawapendi utani, wengine wanapenda sana utani na wengine huonekana wamenuna hata kama wanafuraha. Hivyo ni lazima kuwasoma mmoja mmoja.

Katika maofisi, utakutana na wafanyakazi ambao ni waongeaji, wengine wakimya, wengine wanapenda kucheka pasipo na sababu ya msingi na kila aina ya tabia ambapo ni lazima kila mtu amjue mwenzake ana kasumba na tabia zipi.

Tumia lugha na maneno ya heshima
Epuka sana tabia ya uropokaji usiozingatia lugha nzuri hasa lugha za mitaani. Vijana wengi sana wanashindwa kutofautisha mazingira ya ofisini na mitaani ambpo utakuta maneno anayoyatumia mitaani ndiyo anajaribu kuyatumia hata katika mazingira ya ofisini kwa wafanyakazi wenzake. Jambo ambalo si sahihi.

Kama unashida na mfanyakazi mwenzako, basi mfuate kwa utaratibu kisha muite kwa jina lake ndipo umueleze shida yako.

Katika hili zingatia maneno ya samahani kabla ya kumueleza shida yako.
Na inapotokea umemkosea mfanyakazi mwenzako kwa namna moja au nyingine, basi ni busara kama utamtaka radhi na kutorudia kosa lile.

Sasa utakuta mtu anashida na mfanyakazi mwenzake lakini jinsi anavyomuita na kumueleza, utadhani anamuamrisha mwanaye.

Epuka sana madeni kwa wafanyakazi wenzako na kama ikitokea umekopa fedha kwa mfanyakazi mwenzako basi jitahidi kurejesha kwa muda muafaka, na tena katika hali ya ustaarabu. Pia jitahidi kutoa misaada kwa wenzako wanapopatwa na matatizo.

Kuna wale wenzangu na mimi ambo wao hupenda kusaidiwa tu lakini siyo kusaidia wenzao! Hii ni hatari sana. Jitahidi kuwa karibu na wafanyakazi wenzako kwa kila hali. Kama ni matatizo basi shirikiana nao.

No comments:

Post a Comment