Tuesday, August 16, 2011
KIBABU CHA LOLIONDO HATIMAYE KORTINI
Baadhi ya wagonjwa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi waliokunywa kikombe cha Mchungaji Ambilikile Masapile (pichani) mwaka huu katika Kijiji cha Samunge, Loliondo mkoani Arusha hatimaye wameamua kumburuza mahakamani kiongozi huyo kwa madai kwamba dawa yake haitibu kabisa na wamedanyanywa.
Wakizungumza nyakati tofauti wiki iliyopita kwa sharti la kutoandikwa majina yao, watu hao ambao wako katika Muungano wa Vyama vya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (TANOPHA) walisema kwamba wao ni kati ya waathirika waliopelekwa na chama chao Samunge kupata tiba lakini cha ajabu ni kwamba tangu wanywe dawa hiyo wamekuwa wakipimwa hospitalini na kuonekana kuwa bado wana virusi vya ugonjwa huo.
Waliendelea kusema kwamba kila wakienda kupima ili waone kama wamepona, wamekuwa wakielezwa na daktari kwamba hakuna mabadiliko na kikombe hakijawasaidia lolote lile, hivyo wameona ni udanganyifu na utapeli mkubwa hivyo wameamua kumfikisha mahakamani wakati wowote.
“Hatuwezi kupoteza muda na fedha zetu kwa kwenda kunywa dawa ambayo haitibu, hii ni kuwarubuni wananchi, wengi wameuza mali zao, wengine kutumia akiba ya fedha walizokuwanazo kwenda Loliondo wakijua kwamba wangepona lakini cha kushangaza ni kwamba baadhi yetu wanakufa.
“Wengine wako mahututi baada ya kupewa kikombe, tulikuwa na matumaini ya kupona hadi tuliacha kutumia vidonge vya kurefucha maisha vya ARV, hatuna mengi zaidi ila tunaomba umtafute mwenyekiti wetu akueleza zaidi,” alisema mmoja wa wanachama hao.
NIA YA MWENYEKITI WA TANOPHA
Mwenyekiti wa TANOPHA, Julius Kaaya alipotafutwa kwa njia ya simu juzi ili kueleza madai hayo ya wanachama wake, alisema kwamba ni kweli walipelekwa watu 14 kwenda kunywa dawa Loliondo lakini hakuna hata mmoja aliyepona kwani kila wanapopimwa hospitalini wanaonekana bado wana virusi.
“Nakumbuka kwamba kipindi tunaenda huko Loliondo Machi, 19 mwaka huu tulifanya mkutano na waandishi wa habari, tulifika Samunge Machi 22, ambapo Machi 24 walikunywa dawa hiyo kila mmoja akiwa na matumaini ya kupona, baada ya siku 20 tangu wanywe dawa hiyo walienda hospitali kuangalia kama wamepona, daktari aliwaambia hakuna hata mmoja aliyepona, “ alisema Kaaya.
Aidha, aliendelea kusema kwamba wanachama hao hawakukata tamaa , baada ya siku 90 walirudi tena hospitalini kuangalia kama kuna hauweni, daktari aliwapima na kuwaambia hakuna mabadiliko hata kwa mtu mmoja.
Aliendelea kusema kwamba wanachama hao baada ya kuelezwa hivyo walikata tamaa na kuamua kuendelea kutumia ARV.
“Wengi ambao tunajua kwamba wana HIV na walikunywa kikombe wanapukutika na hata juzi tulihudhuria mazishi ya mmoja wapo, hii dawa haitibu kwani kuna wagonjwa wa kisukari ambao waliinywa hawajapona .
“TANOPHA ina vyama 230 vilivyosajiliwa na mimi ndiye mwenyekiti wao, nimekuwa nikipokea taarifa za baadhi ya wanachama wetu waliokwenda Samunge ambao waliacha kutumia ARV wakijua kwamba wamepona, wengi wamefariki.
“Babu wa Loliondo amedanganywa na shetani na siyo kwamba alielezwa na Mungu, nashangaa viongozi wa dini wanaompigia debe wakati wao siyo wataalamu wa kujua kama dawa hiyo inaponya au la, ni ushabiki wa kidini usiokuwa na maana, lengo lao ni kuchuma fedha kwa wagonjwa.
Kwa nini wasiwaachie wataalamu kushughulikia suala hilo?
“Wanasiasa waliokunywa dawa hiyo na kupigwa picha na vyombo vya habari walihamasisha wananchi kwenda huko kunywa dawa, hawakupaswa kufanya hivyo, wao kama viongozi wangesubiri kwanza wapate matokeo ya utafiti wa Wizara ya Afya.
“Ni kiongozi gani aliyejitokeza na kuonyesha cheti chake hadharani mbele ya vyombo vya habari kwamba amepona, wanaona aibu, ile siyo dawa ni maji tu.
“Wizara ya Afya nao wameingiliwa na wanasiasa ambao wamekuwa wakidai kwamba inatibu wakati Waziri wa Afya kwa upande wake anasema kwamba dawa ya Ukimwi bado haijapatikana duniani.
“Wizara inasema bado wanaendelea kuifanyia uchunguzi hiyo dawa ya Masapile,mpaka lini? Watutajie wangapi walikunywa maana mpaka sasa hakuna idadi kamili, kwa kweli wengi wamefariki ,wengine wako hoi, nawashauri wasiache kutumia ARV.
“Wanaoishi na virusi wasione aibu wajiamini watumie ARV, watambue kwamba ni tatizo limeshawapata na wakifanya hivyo bila kuwa na hofu wanaweza kuishi miaka mingi,” alisema Kaaya.
Alipoelezwa kuwa kuna watu waliokunywa kikombe wanataka kumfikisha mahakamani Mchungaji Masapile, Kaaya alisema hata yeye yupo tayari endapo atampata mtu wa kumsaidia kufungua kesi.
“Masapile ameharibu taifa, ingekuwa kesi inafunguliwa bure kwa kweli ningeshafanya hivyo na kama wanachama wangu wameamua kumfikisha kortini, nawaunga mkono,” alisema Kaaya.
MCHUNGAJI MTIKILA
Naye Mchungaji wa Kanisa la Full Salvation, Christopher Mtikila kwa upande wake amesema kwamba dawa hiyo haitibu na analishughulikia suala hilo ili kumfikisha mahakamani pamoja na mawaziri, wabunge na viongozi wa juu waliokunywa kikombe.
“Mawaziri hao wamewahamasisha wananchi kwenda Loliondo kunywa dawa, lazima tuwashitaki pamoja na viongozi wa dini waliopiga debe,” alisema Mtikila. Viongozi wa dini waliohamasisha ni Askofu Thomas Laizer na Martine Shayo.
Baadhi ya Mawaziri waliopata kikombe ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.Wabunge ni Augustine Mrema, Edward Lowassa na wakuu wa mikoa ni Yohana Balele na Abbas Kandoro.
MAJIBU YA BABU KWA WASIOPONA
Mwandishi wetu wa Arusha wiki iliyopita alizungumza na msaidizi wa Mchungaji Masapile kwa njia ya simu, Paulina Lucas na kuulizwa kuhusu malalamiko hayo akasema wasiopona ni wale ambao hawana imani.
“Kama hawajapona siyo makosa yetu. Tuliwaambia kabla kuwa katika tiba hii kigezo cha kwanza ni kuwa na imani na hapa tuna uthibitisho wa kutosha wa watu walioponywa na maajabu ya dawa hii wakiwemo wagonjwa wenye Ukimwi,” alisema Paulina.
Alidai kuwa kuna baadhi ya watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi si wakweli kwani kuna uwezekano kuwa wamepona lakini wanashindwa kuweka wazi kwa malengo ya kukosa fedha wanazopewa na wafadhili.
No comments:
Post a Comment